Serikali wilayani Njombe imewataka wananchi,wawekezaji na wajasiriamali kote nchini kuchangamkia fursa zinazotarajiwa kuletwa na maonyesho ya kitaifa ya biashara na viwanda vidogo yanayotarajia kufanyika hapo baadae mwaka huu .
Wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maonyesho hayo mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Gwakisa Kasongwa amesema maonyesho hayo yatafanyika katika viwanja vya Saba Saba vilivyopo wilayani Njombe ambapo yanatarajia kuanza tarehe 21 mpaka 31 Oktoba.
Amesema wananchi wa mkoa huo wanatakiwa kutoa ushirikiano kwasababu serikali ya mkoa pamoja Sido mkoa wameanza maandalizi ya tukio hilo kubwa na kuwataka kupokea maonyesho haya kwa mikono miwili.
Amesema mafanikio na muitikio ya wajasiriamali, wadau mbalimbali na wananchi katika maonyesho hayo yameonyesha uhitaji na kupelekea uandaaji wa maonyesho ya nne ya Sido kitaifa yatakayofanyika Njombe na kwamba ni fursa kwa mkoa huo.
Kasongwa anasema wajasiriamali zaidi ya 800 kutoka mikoa mbali mbali Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajia kushiriki huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Pamoja tujenge viwanda kwa uchumi na ajira endelevu.
“Shirika la Sido limekuwa likifanya maadhimisho haya toka 2018 Simiyu,mkoani Singida 2019 kabla ya kwenda Kigoma 2021 na sasa ni zamu ya Njombe,” amesema Kasongwa
Awali akijibu sababu ya kuleta maonyesho hayo Njombe mkurugenzi mkuu wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo nchini SIDO Mhandisi Sylvester Mpanduji amesema ni kutokana uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi Njombe na Kisha kutoa Rai kujikita katika ujasiriamali na uanzishaji wa viwanda vidogo kwasababu kupitia nafasi hiyo watakutana na watu wengine na kubadilishana teknolojia na mawazo.
Prof Mpanduji amesema wakati jitihada za kusaidia wajasiriamali kupitia sido zikiendelea lakini Tanzania bado Ina uhitaji mkubwa wa viwanda vya kuzalisha vifungashio Kama vile chupa na mifuko hivyo watu wachukue hatua ya muwekezaji Huko ili kurahisisha wazalishaji hususani wakulima kupata vifungashio ili kuongeza thamani ya bidhaa zao.
“Rais amekuwa akisema kwamba ni wakati sasa kwa Tanzania kwenda kwenye viwanda kwahiyo tumekuja Njombe ili kuhamasisha wananjombe hii malighafi wanayozalisha itoke kwenye malighafi iwe inauzwa kama bidhaa ambayo imeongezewa thamani,” amesema mhandisi Mpanduji.
Nae Meneja wa SiDO mkoa wa Njombe mhandiai Isdory Kihenze amesema katika maonyesho hayo kutakuwa na teknolojia mbalimbali ambazo zitaweza kutumia pia makaa ya mawe ya Mchuchuma ambayo yanaweza kutumika katika kupikia.
Kuhusu viwanda Kihenze amesema Njombe Ina viwanda zaidi ya 600 lakini viwili pekee ndiyo vinazalisha vifungashio hivyo wawekezaji waitazame changamoto hiyo kama fursa ya kuja kuwekeza.