Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Bw. Adam Mgoi akizungumza Wilayani Bahi mkoani Dodoma Oktoba kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo wakati wa hafla ya uzinduzi na usambazaji wa taarifa ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.
Mtakwimu mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akieleza faida za kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa kutumia mfumo wa kidigitali kwa ajili ya Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi na usambazaji wa taarifa ya kutenga maeneo hayo iliyofanyika Wilayani Bahi mkoani Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamis Munkunda akizungumza Jafo wakati wa hafla ya uzinduzi na usambazaji wa taarifa ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Bw. Wilfred Ochan akieleza kuhusu mikakati ya Shirika hilo kuunga mkono mikakati ya Serikali kufanikisha Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.
Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bi. Elizabeth Talbert akizugumzia umuhimu wa sense na zoezi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Bw. Adam Mgoi akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambapo alimuwakilisha Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kuzindua taarifa ya Wilayani Bahi mkoani Dodoma baada ya kukamilika kwa zoezi za kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ,hafla hiyo iliyofanyika Oktoba 17, 2019 wilayani humo.
………………
Na Mwandishi Wetu- Bahi
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi kwa kutumia takwimu zinazokusanywa ili kuwezesha kupangwa kwa mipango ya maendeleo inayoendana na mahitaji ya wananchi katika huduma za jamii.
Akizungumza Oktoba 17, 2019 huko Bahi mkoani Dodoma wakati wa uzinduzi na usambazaji wa taarifa ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu ya Wilaya ya Bahi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo alisema kuwa taarifa zinazotokana na takwimu zitasaidia katika upangaji wa mipango unaoendana na mahitaji ya wakati.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw. Adam Mgoi, Waziri Jafo alieleza ili kutekeleza dhamira ya serikali ya kuwatumikia vyema wananchi ni lazima kufahamu idadi ya wananchi wake, hali zao za kiuchumi, mahali walipo, elimu yao, afya zao na mahitaji yao ya msingi.
Aliueleza mkutano huo kuwa Takwimu zinazokusanywa wakati wa Sensa ni nyenzo muhimu kwa utayarishaji wa sera za kiuchumi na maendeleo, na inatumika katika kuangalia uboreshaji wa hali ya maisha ya watu.
Alipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar kwa kufanya kazi kwa weledi na ikiwemo kufanya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi miaka mitatu kabla ya zoezi la kuhesabu watu kufanyika kama miongozo ya kimataifa inavyoelekeza.
“Mataifa mengi ya Afrika yanakuja kujifunza hapa Tanzania jinsi Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyotekeleza majukumu yake kwa ufanisi hali iliyowezesha hata kuanza kwa zoezi hili la utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili yan Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022” Alisisitiza Mgoi
Akifafanua amesema kuwa viongozi Viongozi katika ngazi zote hapa nchini wanapaswa kutoa ushirikiano kwa watafiti kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakapokuwa wakitekeleza jukumu la utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu ikiwa ni maandalizi ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 itakayofanyika hapa nchini.
Aliongeza kuwa Sensa hiyo inatarajiwa kufanyika kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA na hivyo kupunguza gharama kuanzia katika hatua za utengaji wa maeneo hadi utekelezaji wa zoezi la sensa mwaka 2022.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt Albina Chuwa aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo kuanza kwa zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Aliongeza kuwa Ofisi yake inapata ushirikiano wakutosha katika mamlaka za Serikali za Mitaa hali inayowezesha kutekelezwa kwa ufanisi kwa zoezi hilo katika Wilaya ya Bahi, Kondoa na Chamwino ambapo kwa Bahi tayari limekamilka pamoja na Sehemu ya Wilaya ya Kondoa.
Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bi Elizabeth Talbert amesema kuwa wataendelea kusaidia juhudi za Serikali katika kufanikisha Sensa ya mwaka 2022 ili kuchochea maendeleo kwa kuwa Benki hiyo hutumia takwimu hizo katika kusaidia miradi ya maendeleo.
Zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 mkoani Dodoma limekamilika katika Wilaya za Bahi na Chamwino pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Vijijini na hivi sasa linaendelea katika Halmashauri ya Kondoa mjini.
Kwa kawaida, Sensa ya Watu na Makazi hufanyika kila baada ya miaka kumi. Sensa ya mwisho kufanyika humu nchini ilikuwa mwaka 2012.