Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera, amezindua tuzo ya malkia wa madini iliyoandaliwa na chama cha wanawake wachimbaji madini nchini (TAWOMA) itakayoshirikisha mikoa 12.
Dk Serera akizindua mchakato wa tuzo za malki wa madini mji mdogo wa Mirerani, ambapo kilele chake kitafanyika mkoani Geita, amewataka wanawake wachimbaji wajitokeze kwa wingi kushiriki.
Amesema ni heshima ya kipekee kwa tuzo hizo kuzinduliwa kwenye madini ya Tanzanite yaliyopo Simanjiro hivyo mwaka ujao wa 2023 TAWOMA waandae tuzo hizo katika wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa TAWOMA, Semeni Malale amesema mshindi wa kwanza atakayenyakua tuzo ya malkia wa madini atapata zawadi ya Sh5 milioni na mshindi wa pili atapata Sh3 milioni.
Amesema mshindi wa tatu atapata Sh2 milioni na mshindi wanne hadi wa 20 watajishindia zawadi zenye thamani ya Sh500,000 kwa kila mmoja.
Makamu Mwenyekiti wa TAWOMA, Rachel Njau amesema wamempatia Mwenyekiti Malale zawadi ya saa ya ukutani na kitabu cha kuandika taarifa mbalimbali ili kumsaidia utendaji kazi wake.
“Hii saa atakuwa anaiangalia ili aweze kuwatumikia wachimbaji wanawake kwa muda sahihi na hiki kitabu kidogo ataandika changamoto na namba za simu za wanachama wake,” amesema Njau.
Katibu wa TAWOMA Salma Kundi ametaja wanawake wa mikoa watakaoshiriki kugombea tuzo hiyo ya malkia wa madini ni Manyara, Shinyanga, Geita, Mwanza, Mara, Tanga na Simiyu.
Kundi ametaja mikoa mingine watakaoshiriki wanawake hao wachimbaji kutafuta malkia wa madini ni Morogoro, Dodoma, Mbeya, Iringa na Singida.
Diwani wa kata ya Mirerani Salome Mnyawi amesema wanawake wafanyabiashara ya magonga walichanga Sh4 milioni na kujenga mfumo wa gesi wa maabara ya shule ya sekondari Tanzanite.
Mwenyekiti wa wanawake wafanyabiashara wa magonja Joyce Mkilanya amesema wamekuwa wanashiriki masuala ya maendeleo kwa ajili ya jamii inayowazunguka mji mdogo wa Mirerani.