Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi ,Wilaya ya Rufiji Ally Maliti ametoa rai kwa wazazi kujenga tabia ya kusema na watoto wao bila kuwaonea aibu ili kujiepusha na vishawishi vinavyochangia kukatisha elimu na ndoto zao.
Aidha amewataka kuwa mstari wa mbele kushirikiana na walimu kufuatilia masomo na malezi yao ili kuleta tija katika kusaidia kupunguza changamoto za kielimu na maadili katika kijami.
Akizungumza wakati wa kikao na viongozi pamoja na wana Jumuiya ya Wazazi Kata ya Mbwara ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Kata Kwa Kata kutembelea jumuiya za Wazazi chama Cha mapinduzi Wilayani Rufiji, alisema elimu ndio nguzo ya maisha kwa vizazi vyetu.
” Tumepokea taarifa juu ya Watoto wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, endapo wazazi tungekuwa tunafuatilia kwa ukaribu watoto hawa masomo yao nyendo zao wasingefika huko”
Chanzo kingine ni sisi wazazi, Hii ni hatari kubwa ni lazima kubadilika, tujenge ukaribu,tuseme nao watoto wetu watimize ndoto zao ” alisema Maliti
Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za Serikali Diwani wa Kata ya Mbwara Juma Ligomba aliipongeza Serikali Kwa kutoa fedha za utekelezaji wa Miradi zaidi ya shilingi Bilioni Moja Kwa Kata hiyo.
Aidha alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utaliii Mohammed Mchengerwa Kwa namna ambavyo anajitoa kupigania Maendeleo ya Wilaya ya Rufiji hususani Kata ya Mbwara ambayo Ilikuwa ikikabiliwa na changamoto, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara ambayo hadi Sasa zaidi ya kilometa nane tayari zimefanyiwa matengenezo na barabara kupitika kwa urahisi.
Nae Mjumbe wa Mkutano Mkuu Wazazi Taifa ,Fatima Msumi aliwataka Wazazi kuzungumzia maswala ya malezi na ujinsia Kwa Watoto hususani changamoto za mmonyoko wa maadili ikiwemo madhara ya mahusiano ya jinsia Moja Kwa Watoto wa kiume na usagaji Kwa Watoto wa kike.
“Tusikae kimya Kwa kufikiri kuwa changamoto hizi ni za nje ya Wilaya yetu hata kwetu zipo Tuzungumze na kuwalinda Watoto wetu.” alisisitiza. Fatuma.
Vilevile Jumuiya hiyo imetoa kadi Kwa Wanajumuiya 1,300 na kutembelea Wagonjwa Hospital ya Wilaya, kituo Cha Afya Mohoro na kutoa misaada na zawadi ya Baskeli Moja ya walemavu, sabuni za maji, unga , Sukari na taulo za kike kwa Watoto wa kike Shule ya Msingi Mohoro na Shule ya Sekondari Utete, Mkongo na Mwaseni Wilayani Rufiji.