Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke (katikati),akizungumza kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa BAKWATA wa kupokea taarifa ya maandalizi ya sherehe za Maulidi ya Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika jijini Mwanza Novemba 9, mwaka huu.
Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Maulidi ya Mtume Muhammad S.A.W. Sadiki Mshola akitoa taarifa fupi ya fedha za maandalizi kutoka vyanzo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Miundombinu na Mapambo, Musa Mkumbi, akitoa taarifa kwenye mkutano Mkuu Maalum wa BAKWATA mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhusu hatua iliyofikiwa pamoja na bajeti inayohitajika.
****************************
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
WAUMINI wa Dini ya Kiislamu Jiji la Mwanza wameaswa kulinda amani, utulivu na usalama wa nchi pamoja na wageni wakati wote wa sherehe za Maulidi ya Mtume Muhammad S.A.W, kwani amani ikivunjika wote watahusika.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Masheikhe wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Haruna Kichwabuta, kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa BAKWATA kwa niaba na masheikhe hao wakati wa kupokea taarifa ya maandalizi ya maulidi uliofanyika,kwenye Ukumbi wa Sheikhe Salum Ferej.
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Kagera, alisema suala la amani na utulivu ni muhimu, lakini ikivunjika waislamu wote watahusika,hivyo lazima wajichunguze na kuwachunguza wengine wenye nia ovu wanaoweza kujipenyeza ili kuvuruga amani, utulivu ili kuharibu jina la Uislamu na Maulidi yenyewe.
“Waislamu tuhakikishe tunakuwa macho na watu wenye nia ovu wanaoweza kujipenyeza miongoni mwetu wakati wa Maulidi ili kuchafua Uislamu.Tunahitaji watu watakaokuja hapa watusaidie kulinda amani na utulivu wa nchi yetu na kuhakikisha usalama unakuwepo.Pia tutakuwa na wageni , tuwaangalie na kusimamia usalama wao licha ya kuwepo kwa vyombo vya ulinzi na usalama,”alisema Sheikhe Kichwabuta.
Alisisitiza kwa vile waislamu wanayo dhamana kubwa ya kulinda amani na utulivu wahakikishe sherehe hizo za kihistoria za maulidi ya Mtume S.A.W. yanafanyika kwa amani, usalama, mshikamano na upendo miongoni mwa waumini Kiislamu na jamii ya Watanzania.
Sheikhe Kichwabuta pia ahimiza waumini kushiriki na masheikhe kuendelea kusema na kukutangaza jambo hilo la heri kwenye mimbari (msikitini) na kushughulika na watu wanaoyahitaji maulidi,waachane na wasiyoyataka ili mwisho wa siku yafanyike kulingana na hadhi ya Jiji la Mwanza.
Aidha, Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza alhaji Hasani Kabeke alisema Kitendo cha Mufti Abubakar Zuberi kuipa BAKWATA mkoani humu jukumu la kuandaa Maulidi ya Mtume S.A.W. Kitaifa baada ya miaka 29 ni mtihani, ili kuufaulu ni kuyafanikisha.
Alisema kwa sababu Watanzania waislamu na wasio waislamu wanashirikiana kwa mambo mbalimbali ya kijamii, washirikiane kwa wenye uwezo,wajitoe hali na mali, wenye magari ama nyumba za wageni wasaidie kuwahifadhi wageni hao wa Mtume S.A.W. na kuwasafirisha.
Tunashirikiana na waislamu na wasio waislamu, hivyo wasio waislamu hawajaweewa pazia (mipaka), wanayo haki ya kuchangia Maulidi.Wajitokeze na watusaidie kuwahudumia wageni wa Mtume Muhammad S.A.W. na si BAKWATA.Watakachotoa ni kwa ajili ya wageni hao wa mtume,”alisema.