Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akiwasha umeme katika Sekondari ya Shambarai iliyopo katika Kijiji cha Nakweni wilayani Simanjiro ikiwa ni ishara ya kuwasha rasmi umeme kwenye kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akikata utepe kuashiria kuwasha rasmi umeme katika Kijiji cha Naepo wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara. Wa Tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Eng. Zephania Chaula na wa Pili kushoto ni Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya.
Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Nakweni wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara mara baada ya Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kulia kwa Mbunge) kufika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme. Kushoto kwa Mbunge ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Eng. Zephania Chaula.
Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Naepo wilayani Simanjiro wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) aliyefika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme na kuwasha rasmi umeme kwenye kijiji hicho.
Baadhi ya miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Nakweni wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akivishwa vazi maalum la kimasai na kupatiwa fimbo maalum mara baada ya kufika katika Kijiji cha Naepo wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara ili kuwasha rasmi umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akiagana na wananchi katika Kijiji cha Nakweni wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara mara baada ya kuzungumza nao kuhusu kazi ya usambazaji umeme kwenye Kijiji hicho. Dkt Kalemani pia aliwasha rasmi umeme kwenye Kijiji husika.
………………
** Atoa agizo kwa viongozi
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameeleza kusikitishwa kwake na suala la Taasisi za umma na maeneo yanayotoa huduma za kijamii kutounganishiwa umeme katika baadhi ya vijiji nchini huku nishati hiyo ikiwa tayari imefika kwenye vijiji hivyo.
Dkt. Kalemani aliyasema hayo tarehe 16 Oktoba, 2019, wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara wakati alipofanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini na kuwasha umeme kwenye baadhi ya vijiji akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Eng. Zephania Chaula, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya na watendaji kutoka TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Awali, taarifa ya TANESCO katika Wilaya ya Simanjiro ilieleza kuwa, mkandarasi wa umeme vijijini wilayani humo, tayari amewasha umeme katika vijiji 11 kati ya 21 alivyopangiwa lakini ni Taasisi chache za umma zimeunganishwa na umeme.
” Ina maana baadhi ya viongozi wa Vijiji na Halmashauri hawalipii umeme ili taasisi za umma na maeneo yanayotoa huduma za kijamii kama visima vya maji yaunganishiwe umeme, itabidi ifike mahala tuulizane na viongozi hawa kwa nini hawalipii umeme kwenye Taasisi zao.” alisema Dkt Kalemani.
Kutokana na hilo, Dkt Kalemani aliendelea kuwasisitiza viongozi hao kote nchini, kutenga fedha za kuunganisha umeme kwenye taasisi hizo ili umeme huo uweze kuleta tija kwa jamii.
Kuhusu usambazaji umeme wilayani Simanjiro, Dkt Kalemani alisema kuwa, Wilaya hiyo ina vijiji 56 na tayari vijiji 39 vimesambaziwa umeme ambapo aliagiza kuwa, ifikapo mwezi Disemba mwaka huu, vijiji vyote vilivyosalia viwe vimesambaziwa umeme.
Aidha, akiwa wilayani humo, Dkt Kalemani aliwasha umeme katika Kijiji cha Naepo na Nakweni ambapo aliagiza kuwa vitongoji vya Vijiji hivyo ambavyo havina umeme, visambaziwe umeme.
Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, alimshukuru Rais, Dkt John Pombe Magufuli kwa kazi inayofanyika ya usambazaji umeme vijijini na kueleza kuwa juhudi hizo zimepelekea umeme kusambaa katika maeneo mbalimbali nchini
Aidha, alimshukuru Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini bila kubagua maeneo na kueleza kuwa Wilaya hiyo imefaidika na miradi ya umeme vijijini kwani takriban asilimia 70 ya vijiji wilayani humo, tayari vina nishati ya umeme.