Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imesema kuwa inatambua kuwa ndoa ni kati ya mwanaume na mwanamke.
Hayo yamesemwa leo Mei 22,2023 Jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro wakati akifungua kikao cha mashauriano kati ya Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) na Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya mabadiliko yanayopendekezwa ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.
“Kwa wanasheria wanasema ndoa ni makubaliano kati ya mwanamke na mwanaume. Na hii inatokea kwenye tamko la haki za binadamu (Universal Declaration of Human Right) ambalo linatambua ndoa ni kati ya mume na mke, haya mengine yanayotokea haya yanaitwa ndoa lakini ukisoma tamko hilo hazina sifa za kuitwa ndoa,” amesisitiza Waziri Ndumbaro.
Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa tamko hilo lilitolewa mwaka 1948, miaka mitatu mara baada ya kuundwa kwa Umoja wa Taifa na kuongeza kuwa tamko hilo ndio katiba ya haki za binadamu duniani.
Akizungumza mapema Mkurugenzi wa WISE, Dk. Astranout Bagile amesema kuwa ni muhimu sheria ya ndoa ikafanyiwa marekebisho kutokana na uzito wa majukumu ya kulea familia na kuongeza kuwa mmomonyoko wa maadili kwa sasa unaweza kuwa unasababishwa na watoto kupewa majukumu ya kulea watoto wenzao kutokana na kuolewa katika umri mdogo.
Kikao hicho cha Mashauriano kimehudhuriwa na Mkurugenzi wa WiLDAF,Wakili Anna Kulaya.