SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dk Tulia Ackson,akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Mhandisi Peter Ulanga wakati alipotembelea banda la Shirika hilo katika Maonesho yanayoendelea viwanja vya Bunge Jijini Dodoma leo Mei 18,2023.Kushoto ni Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo.
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dk Tulia Ackson,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mabanda mbalimbali katika Maonesho yanayoendelea viwanja vya Bunge Jijini Dodoma leo Mei 18,2023.
Meneja Biashara TTCL Dodoma Bi.Leyla Pongwe,akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la shirika hilo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Mhandisi Peter Ulanga wakati katika Maonesho yanayoendelea viwanja vya Bunge Jijini Dodoma leo Mei 18,2023.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Dk Tulia Ackson amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kufanya vizuri katika utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja na kufikisha huduma za mawasiliano ya intaneti kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Pongezi hizo amezitoa leo Mei 18,2023 wakati alipotembelea banda la Shirika hilo katika Maonesho yanayoendelea viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.
Spika Tulia amesema ameoneshwa mambo mengi katika banda la TTCL lakini suala la mkongo kufika nyumbani ni jambo la muhimu kwani matumizi ya data na teknolojia ni muhimu.
“Nitume nafasi hii kuwapongeza TTCL kwa kutuleta huduma hii naamini zitapunguza gharama ya matumizi ya bando ambayo tumekuwa tunalalamika.
“Tumeona mmefika Kilimanjaro,hiyo itakuwa nzuri kwa sababu kutakuwa hakuna uongo uongo,piga tujue umefika kileleni kama mmefika pale ni vizuri nawaongeza sana mnafanya kazi nzuri,”amesema Spika Tulia.
Kuhusu zoezi la anuani za makazi,Spika Tulia amesema : “Nimefurahi kuona zoezi hili la anuani ya makazi ambalo limeanza mapema mwaka jana na sasa tumefikia sehemu yule ambaye amesajiliwa anuani yake anaweza kupata huduma kwa kutumia simu yoyote,”.
Kwa upande wake Meneja Biashara TTCL Dodoma Bi.Leyla Pongwe amesema wamefika bungeni kuwaonesha wabunge mikakati ambayo wanayo katika kuisaidia serikali kwenye kuchagiza kufikia uchumi wa kidigital mpaka mwaka 2025.
Amesema wanajivunia kwa sasa kwani wameweza kufikisha huduma ya intaneti katika mlima Kilimanjaro.
“Zamani ilikuwa mtalii akipanda juu anakuwa hapatikanai ila sasa hivi mtalii anapatikana.Sasa hivi tunamletea mtanzania fiber mpaka nyumbani kwake analipia kifurushi kwa mwezi kwani ili kufikia uchumi wa kati lazima uwe na intaneti,”amesema meneja huyo.
Amesema wamewaonesha wabunge ukiwa na intaneti Fiber ya TTCL unaweza kuwasaliana hata ukiwa mbali mradi una intaneti popote ulipo na unawea kufanya kwa kupitia application ya simu.
Amesema wameweza kufikisha mkongo wa Taifa mpaka katika maeneo ya mipakani mwa Tanzania na sasa hivi wanaanza kutoka nje ili kufikisha mawasiliano katika Nchi zote za jirani
“Tunakituo cha data centre ambacho kinatumika kutunza taarifa na data za watoa huduma na serikali tunawaribisha watu wote kutunza kumbukumbu zao,”amesema