WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu,Dkt.Dorothy Gwajima,akiwasilisha bajeti ya Wizara yake leo Mei 18,2023 bungeni,Jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna_DODOMA
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu,imewasilisha bajeti bungeni huku ikitaja vipaumbele 10 itakavyovitekeleza kwa mwaka 2023-2024.
Wizara hiyo inaliomba Bunge kuiidhinishia jumla ya zaidi ya Sh bilioni 74 ili kutekeleza majukumu yake kwa maendeleo na ustawi wa jamii.
Akiwasilisha bajeti hiyo leo Mei 18,2023 bungeni,Jijini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo,Dk Doroth Gwajima amevitaja vipaumbele hivyo ni kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi (Generation Equality Forum – GEF).
“Kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA),kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi wa mwaka 2022/23 – 2025/26 (Bottom Up),”amesema Dk Gwajima.
Amevitaja vipaumbele vingine ni kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo,kutambua na kuratibu Makundi Maalum wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo ili kuboresha mazingira ya biashara zao.
“Kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii,kuimarisha mifumo ya malezi, ulinzi na maendeleo ya watoto na familia,”amesema Waziri huyo
Vilevile kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum ikiwemo huduma za msaada wa kisaikolojia kwa manusura wa majanga mbalimbali na makundi mengine yenye uhitaji katika jamii 109.
“Kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa haki za watoto na huduma za ustawi wa jamii kwa wazee na kuimarisha utendaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali,”amesema Waziri Gwajima.
KUTUMIA BILIONI 74 KUTEKELEZA VIPAUMBELE
Waziri Gwajima amesema katika kutekeleza vipaumbele hivyo Wizara kwa mwaka 2023/24 imekadiria kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 74.2 zitakazotumika kutekeleza majukumu ya Wizara ikiwa ni pamoja na kuwezesha uendeshaji wa ofisi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ameitaja baadhi maeneo yaliyotengewa fedha kwa mwaka 2023/24 ni pamoja na Katika eneo la kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi (Generation Equality Forum – GEF) ambapo kiasi cha shillingi bilioni 4.9 zimetengwa kwa ajili ya kuratibu shughuli hizo.
Amesema katika eneo la kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3 kimetengwa.
BILIONI 18 MIKOPO KWA MACHINGA
Amesema katika eneo la kutambua na kuratibu shughuli za kiuchumi za Makundi Maalum hususan wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo machinga, mama/baba lishe, waendesha bodaboda na bajaji, kiasi cha Shilingi Bilioni 18.5 kimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuongeza mitaji na kuboresha shughuli zao za kiuchumi.
WATOTO
Amesema kwenye eneo la watoto, kiasi cha Shilingi Bilioni 3.6 kimetengwa kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na marekebisho ya tabia kwa watoto waliokinzana na sharia.
“Kufuatilia utoaji wa huduma katika Makao ya Watoto, Nyumba Salama na Vituo vya Kulelea Watoto wadogo Mchana na Watoto Wachanga; Kukarabati Shule ya Maadilisho ya Irambo; Kukarabati Mahabusu za Watoto Upanga, Arusha, Mbeya, Moshi na Tanga; na Kukamilisha ujenzi wa Mahabusu ya Watoto Mwanza,”amesema Dk Gwajima.
WAZEE
Amesema katika eneo la wazee, Shilingi Bilioni 1.8 zimetengwa kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa huduma za ustawi kwa wazee wasiojiweza katika Makazi ya Wazee 14 na ukarabati wa majengo na miundombinu 111 katika Makazi ya Misufini, Mwanzange, Ipuli na Bukumbi.
Waziri huyo amesema kwenye eneo la taasisi na Vyuo, kiasi cha Shilingi Bilioni 3.1 kimetengwa.
Amesema Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo na miundombinu katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, na Vyuo vitatu (3) vya Maendeleo ya Jamii vya Uyole, Monduli na Misungwi.
URATIBU WA NG’OS
Kwenye eneo la Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali amesema limetengewa kiasi cha Shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya ufuatiliaji wa Mashirika 1,000 katika Kanda Tano, kusajili Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yapatayo 1,000.
Pia kuandaa taarifa ya Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka 2022, kuwezesha Mfumo wa Kielektroniki wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NIS), kuratibu utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2022/2023 – 2025/2026).
Vilevile kuratibu Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kuratibu Vikao vya Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
MAENDELEO YA JAMII
Waziri Gwajima amesema eneo la maendeleo ya jamii limetengewa kiasi cha Shilingi Milioni 283.6 kwa ajili ya kutekeleza Kampeni.
“Kuamsha ari ya jamii kuhusu ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu kwa kutumia teknolojia rahisi na kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi wa mwaka 2022/23 – 2025/26 (Bottom Up) katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara,”amesema Waziri huyo.
Amesema katika eneo la ufuatiliaji na tathmini, kiasi cha Shilingi Milioni 200 kimetengwa ambapo fedha hizo ni kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa mipango, programu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Taasisi, Vyuo na Vituo vya Ustawi wa Jamii vilivyo chini ya Wizara.
MAKUNDI MAALUM
Dk Gwajima amesema Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia mipango na programu mbalimbali za kuwezesha na kuendeleza kiuchumi Makundi Maalum.
Amesema makundi yanayolengwa ni Wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo Machinga, Mama/Baba Lishe, Waendesha Bodaboda na Bajaji ambao hupata changamoto kuzifikia fursa zilizopo kujikwamua na kukua kiuchumi kutoka kwenye taasisi za fedha kwa kuwa hawatambuliwi rasmi na pia hawana dhamana za kuwawezesha kukopesheka kwenye taasisi hizo.
HAKI YA MAENDELEO YA MTOTO
Waziri huyo amesema Wizara inaendelea kuratibu na kusimamia utoaji wa haki za msingi kwa mtoto ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa.
Hata hivyo, baadhi ya watoto hawazipati haki hizo na hivyo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili katika familia na jamii.
“Nitoe wito kwa jamii kuendelea kujitokeza mbele ya vyombo vya utoaji haki kutoa ushahidi ili kesi zote zilizopo kwenye mnyororo wa haki jinai ziweze kufika mwisho na haki ipatikane,”amesema Dk Gwajima.
HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII
Dk Gwajima amesema Wizara ina jukumu la kusimamia, kuratibu na kutoa huduma za ustawi wa jamii hapa nchini zikiwemo haki, matunzo na ulinzi kwa wazee, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Pia watoto walio katika mkinzano na sheria, huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia na wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu, huduma za msaada wa kisaikolojia katika jamii, uratibu wa huduma za afya kwa makundi maalum.
Vilevile huduma kwa familia duni, usajili na usimamizi wa makao na vituo na makao ya kulelea watoto nchini, uratibu wa huduma za malezi ya kambo na kuasili na utatuzi wa migogoro ya familia na ndoa.
Amesema Majukumu hayo yanatekelezwa na wataalam wa ustawi wa jamii kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mahsusi inayoongoza utoaji wa huduma za ustawi wa jamii nchini.
“Natoa wito kwa jamii kuendelea kuwatumia wataalamu wa Ustawi wa Jamii katika ngazi zote pale wanapobaini mienendo mibaya ya tabia ya watoto katika maeneo wanayoishi ili wafanye ufuatiliaji kabla ya watoto hao kuingia katika hatari za kukinzana na sharia,”amesema waziri huyo.
MAENDELEO YA WANAWAKE
Dk Gwajima amesema Wizara katika kukuza usawa na uwezeshaji wanawake, inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Utekelezaji wa ahadi za Nchi kuhusu Jukwaa la Kizazi chenye Usawa 2021/22 – 2025/26 62 (Generation Equality Forum Commitments) ambalo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kinara wa utekelezaji wa eneo hilo.
Amesema utekelezaji wa programu hiyo unajumuisha afua za kuanzisha na kuendeleza vituo vya malezi na makuzi ya watoto, kuongeza uwekezaji katika usambazaji wa maji, umeme na nishati mbadala yenye kutunza mazingira na matumizi ya teknolojia yenye gharama nafuu na inayofaa katika kutatua changamoto za majukumu mengi kwa wanawake katika maeneo ya vijijini na mijini.
Pia, kuongeza kazi zenye staha kwa kuendeleza biashara na urasimishaji wa biashara za wanawake na kuboresha upatikanaji na matumizi ya teknolojia nafuu na zinazofaa ili kuongeza uwezo wa wanawake wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani wa soko la ndani na nje.