Na. Catherine Sungura-Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya imeagiza mashine Tiba (thermocoagulators) 100 zaidi ambazo zinatarajiwa kusambazwa kwenye vituo vya kabla ya mwezi Disemba 2023. Upatikanaji wa vifaa tiba hivyo utaenda kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya matibabu ya Saratani ya mlango wa kizazi katika vituo 100 zaidi vya ngazi ya msingi ikiwemo hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati katika mikoa 13 inayoongoza kwa tatizo la saratani ya mlango wa kizazi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2023/2024 kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.
Waziri Ummy alisema licha ya kuagiza mashine hizo pia Wizara kwa kushirikiana na Wadau imenunua mashine tiba (thermocoagulators) 50 zinazotibu mabadiliko ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi na kusambazwa katika vituo 50 vya kutolea huduma za afya nchini na watoa huduma wameshajengewa uwezo namna ya kuzitumia.
“Upatikanaji wa vifaa vifaa tiba hivi utaenda kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya matibabu ya Saratani ya mlango wa kizazi katika vituo vya afya na zahanati katika mikoa 13 inayoongoza kwa tatizo la saratani ya mlango wa kizazi”.
Katika huduma za kuzuia na kukinga Saratani za mfumo wa uzazi (Reproductive cancers) zikiwemo Saratani ya Mlango wa kizazi na Saratani ya matiti. Katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 wanawake wapatao 426,774 walifanyiwa uchunguzi wa Saratani ya mlango wa kizazi na kati yao wanawake 13,721 sawa na asilimia 3.2 waligundulika kuwa na mabadiliko ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi, ikilinganishwa na asilimia 3.1 mwaka 2021/22.
Aidha, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, 2023, Wizara imefanikiwa kuanzisha vituo vipya 122 vya kutoa huduma za uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na hivyo kufikia jumla ya vituo 923 ikilinganishwa na vituo 801 mwaka 2021/22.
Kwa upande wa udhibiti wa Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza (Non Comunicable desease-NCDs), Waziri huyo alibainisha kwamba kumekuwa na ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ulimwenguni kote ikiwemo Afrika na Tanzania kwa ujumla. Magonjwa haya ni pamoja na Magonjwa ya Moyo, Figo, Shinikizo la juu la damu, Saratani, Kisukari, matatizo sugu ya mfumo wa upumuaji, ajali (injuries), afya ya akili na madawa ya kulevya.
“Magonjwa haya yanabakia kuwa ndio sababu kuu ya madhara na vifo. Miongoni mwa vyanzo vikuu vinavyohusishwa na ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na, ulaji usiofaa, matumizi ya tumbaku, kutoshughulisha mwili (kazi zinazotumia nguvu) na matumizi ya pombe kupita kiasi”.Aliongeza
Vilevile alisema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamesababisha wagonjwa wengi kuhudhuria vituo vya kutolea huduma za afya ni pamoja na shinikizo la juu la damu wagonjwa 890,788 sawa na asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.6 kipindi kama hicho mwaka 2021/22 na kisukari wagonjwa 436,232 sawa na asilimia 1.8.
“Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi hicho, ugonjwa uliongoza katika kusababisha vifo vingi kati ya magonjwa yasiyoambukiza ulikuwa ni ugonjwa wa Moyo ambao ulisababisha vifo 1,388 sawa na asilimia 6.0 ya vifo vyote, ikilinganishwa na asilimia 5.4 ya vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huo kipindi kama hicho mwaka 2021/22. Hali hii inaonesha magonjwa yasiyoambukiza yasipodhibitiwa yanaweza kusababisha ongezeko kubwa la vifo nchini”.
Hata hivyo, Wizara imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kujikinga na Magonjwa yasiyoambukiza ambapo katika kipindi cha Julai 2022 hadi 72 Machi, 2023 jumla ya watumishi 1,690 katika vituo vya afya 497 vilivyopo katika halmashauri 120 wamepatiwa mafunzo kuhusu kugundua na kutibu magonjwa haya kwa ufanisi, lengo likiwa ni kuzifikia Halmashauri zote hapa nchini kufikia Desemba, 2023.
Pia Wizara imenunua na kusambaza mashine maalum ikiwemo Mashine 700 za Kupima shinikizo la damu, vifaa 700 vya kupima mapigo ya Moyo, mashine 2,000 za kupima sukari, vifaa 700 vya uchunguzi wa saratani, mizani 700 za kupima uzito na urefu na vifaa vingine vya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kwenye ngazi ya msingi.