Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MWENGE wa uhuru umepokelewa Mkoani Pwani, kutoka Mkoa wa Morogoro ambapo ukiwa Mkoani hapo utapitia Miradi 96 yenye thamani ya trilioni 4.4 .
Akipokea Mwenge huo , eneo la Ubena Estate Mkuu wa Mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, anaeleza kati ya miradi hiyo miradi 55 itakaguliwa,Tisa itafunguliwa ,15 itazinduliwa na 20 itawekwa mawe ya msingi .
“Miradi hiyo inadhihirisha kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan “
Vilevile Kunenge alielezea kuwa, kwa kutambua umuhimu wa Utunzaji wa Mazingira na Vyanzo vya maji ,wanahakikisha shughuli zote zinafanyika kwa kufuata matakwa ya sheria ya Mazingira 2004 kifungu 57.
“Katika Utunzaji wa Mazingira Mkoa unadhibiti ukataji holela wa Mkaa na kukata miti pamoja na kuimarisha ulinzi dhidi ya ukatiji miti holela kwenye vyanzo vya maji kwa kufanya Ulinzi wa mara kwa mara.”
Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani, amekabidhi mwenge wa Uhuru katika Halmashauri Chalinze, ambapo Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Halima Okash alifafanua, mwaka uliopita Halmashauri hiyo iliongoza kwa kuwa ya kwanza kitaifa .
Okash anasema, Mwenge huo utapitia miradi 23 wilaya ya Bagamoyo kati ya hiyo miradi 14 yenye thamani ya Bilioni 2.4 itapitiwa Halmashauri ya Chalinze na miradi 11 ya sh.Bilioni
2.3 Halmashauri ya Bagamoyo .
Akiweka jiwe la msingi katika upanuzi wa mradi wa maji Mtambani , mradi ambao unatekelezwa na Wakala wa usambazaji maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA, chini ya mkandarasi mzawa Josan Engineering Group, Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa (2023), Abdallah Shaib , alisisitiza kutunza Mazingira na Vyanzo vya maji ndani ya jamii.
Meneja wa RUWASA Bagamoyo James Kionaumela,alieleza mradi huo una thamani ya milioni 176.3 , chanzo cha fedha ni kutoka fedha za lipa kwa matokeo (PbR) ambazo zilitolewa kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya maji.