Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, akizungumza na waandishi wa habari.
Na Mwandishi wetu, Arumeru.
BODI ya bonde la Pangani imepanda miti 1,000 kwa ajili ya kuzuia mmomonyo wa ardhi ili kulinda kingo za mtaro unaosafirisha maji hadi mto Nduruma na Kikuletwa Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
Baadhi ya wakulima na wakazi wa kata ya Shambarai Burka na Mbuguni wilayani Arumeru wamenufaika na mtaro huo wa kilometa 18 uliochimbwa na bonde la Pangani.
Miti hiyo 1,000 imepandwa ili kulinda kingo za mtaro huo usimomonyoke na kuepusha adha ya mafuriko iliyowatesa muda mrefu wakazi hao kwa nyumba na mazao kusombwa na maji.
Mkuu wa wilaya Arumeru, Emmanuela Mtatifikolo Kaganda ameongoza shughuli ya upandaji miti hiyo 1,000 ili kulinda mazingira ya eneo hilo na kupiga marufuku kilimo cha pembezoni.
Kaganda wakati wa utekelezaji wa shughuli hiyo ameshuhudia uharibufu wa miondombinu hiyo kwa baadhi ya wananchi kuvamia eneo hilo na kuanza kufanya kilimo.
Hata hivyo, Kaganda amewapiga marufuku wakulima waliovamia na kuanza kulima hivyo upandaji wa miti hiyo utakomesha changamoto hiyo ya uvamizi wa mtaro huo.
“Wote waliovamia eneo hili waondoke mara moja na endapo watarudia tena kufanya kilimo pembezoni mwa mtaro huu tutawachukulia hatua kali za kisheria,” amesema Kaganda.
Amesema licha ya changamoto zilizojitokeza mapema, ukiachilia upandaji miti, bodi ya maji bonde la Pangani imefanya vyema kwa kulinda na kutunza miundombinu hiyo.
“Bonde la Pangani wameshafanya kazi yao kubwa ya kudabua mtaro, tunapaswa kuwaunga mkono kwa hilo tukitambua jukumu kubwa linabaki kwetu wakazi wa hapa,” amesema.
Mkazi wa kijiji cha Migungani, Iddy Salimu amesema baadhi ya wakulima waliovamia eneo hilo na kulima pembezoni mwa mtaro huo wanapaswa kupewa onyo kali ili wasirudie.
Mwenyekiti wa kijiji cha Shambarai Burka, Mohamed Juma amesema aabaada ya kutokea kwa uharibifu huo wa mapema wameandaa mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
Mtaro huo una urefu wa kilometa 18 na kabla ya kufanyika kwa udabuaji huo wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wahanga wa mafuriko kwa muda mrefu, kama kupoteza maisha, kusimama kwa shughuli za kilimo, wanafunzi kusitisha masomo kwa muda na wengine kulazimika kikimbia makazi yao.