Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Willium Mahalu akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kambi maalum ya matibabu ya siku saba inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel hivi karibuni katika ukumbi wa Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Willium Mahalu akipokea mashine ya kupima jinsi moyo unavyofanya kazi “Echocardiography” iliyotolewa na shirika la SACH na kukabidhiwa na Mjumbe wa bodi ya Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la nchini Israel Riva Grinshpan wakati wa mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni katika ukumbi wa Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaaam.
Madaktari, wauguzi, na mafundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), na wenzao kutoka shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la nchini Israel katika picha ya pamoja na wazazi na watoto waliofanyiwa upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa cath lab katika kambi maalum ya siku saba inayofanywa na madaktari hao.
Picha na: JKCI
………………………
Na: Genofeva Matemu – JKCI
Katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete imepokea mashine ya kupima jinsi moyo unavyofanya kazi “Echocardiography” yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 120 kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Canada.
Akipokea mashine hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Willium Mahalu amelishukuru shirika la SACH Canada kwa kuendelea kuwa wawezeshaji wa taasisi ya SACH Israel pamoja na kuwaleta madaktari, kuleta vifaa tiba na kutoa mashine ya Echocardioghraphy kwaajili ya matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa JKCI.
“Tunaishururu taasisi ya SACH kwa kutupatia mashine ya Echocardiography maana kwa sasa tuna watoto wengi mikoani wanaumwa magonjwa ya moyo na hawawezi kufika JKCI, hivyo tutaitumia mashine hii kuwafuata wagonjwa mikoani kutokana na mashine hii kuwa na uwezo wa kuhamishika” alisema Prof. Mahalu
Aidha Prof. Mahalu alisema kuwa mashine ya Echocardiography iliyotolewa na SACH imekuja kwa wakati muafaka kwani kwa sasa JKCI imeanzisha programu za kwenda mikoani kuwafanyia uchunguzi wananchi wasioweza kufika JKCI hivyo kurahisisha matibabu kwa watoto wenye magonjwa wa moyo waliopo mikoani.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mashine hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) kutoka nchini Canada Marni Brinder amesema kuwa SACH Canada imedhamiria kushirikiana na JKCI kutoa huduma bora za matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo Tanzania ili wawe na maisha yenye furaha.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Naiz Majani amesema kuwa mashine ya Echocardiography ni kifaa muhimu katika matibabu ya moyo kwani asilimia 95 za magonjwa ya moyo zinaweza kutambulika kwa kutumia mashine hiyo, kadhalika hutumika kama kipimo cha awali kugundua kama mtu ameathirika na magonjwa ya moyo.
Hii ni mara ya sita kwa madaktari kutoka shirika la SACH kuja hapa nchini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na madaktari wa JKCI.