Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuipatia fedha nyingi sekta ya kilimo huku akishauri kufanyiwa uchambuzi watu watakaoshiriki kwenye uwekezaji wa viwanda vya kubangua korosho.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka 2023/24, Chikota amesema maono hayo yamechangia bajeti kufikia Sh.Bilioni 970 na matarajio ya wakulima kwamba sekta hiyo italeta manufaa ambayo wabunge walikuwa wakiyalilia kila mwaka.
Akizungumzia uongezaji wa thamani wa zao la korosho, Mbunge huyo amesema kuna tatizo la bei ndogo kwa mkulima na haina tija ambayo kwa miaka miwili kwenye minada sasa wakulima hawapati bei yenye tija.
“Kuna utitiri wa makato na tozo ambayo inapunguza bei kwa mkulima, lakini ni zao pekee ambalo lina export levy ambayo inapunguza bei kwa mkulima,”amesema.
Amepongeza Wizara kwa kuja na mwarobaini kwa kutenga fedha Sh.Bilioni 10 ili zipelekwe sekta binafsi kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kubangua korosho.
“Hili ni suluhisho la kuuza korosho ghafi kwa kuwa tukiendelea kuuza wakulima wetu hawatafaidika lakini tukiuza korosho karanga watanufaika,”amesema.
Hata hivyo, amemtahadharisha Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuwa dhamira hiyo itaibua vita ya kibiashara kwa kuwa kuna nchi hazipendi Tanzania kuuza korosho karanga na kuomba kuwepo na maandalizi ya kutosha.
“Hao tutakaowashirikisha kwenye sekta binafsi wawe na nia ya kuwekeza kubangua korosho Tanzania, kwasababu tuna uzoefu wa viwanda 12 lakini baada ya muda mfupi vilifungwa na vilibinafsishwa hadi leo viwanda ni magodaoni, lazima tufanye vetting ya tutakaokuwa nao kwenye uwekezaji bila hivyo yatatukuta ya zamani,”amesema.
Pia, ameshauri wawekezaji hao kupewa motisha kwa kupunguza kodi kwenye mitambo inayoingia ili kupata wawekezaji watakaofanya uwekezaji mzuri.
Kuhusu umwagiliaji, Mbunge huyo amesema kuna bonde la Ruvuma bado halijatumika ipasavyo na kuomba mkandarasi aliyepewa kazi ya kufanya usanifu aanze Songea hadi Wilaya ya Mtwara.