Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali imesema kuwa itaendelea kuimarisha sekta ya kilimo nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha Kilimo Anga.
Akizungumza leo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema kuwa wizara yake imeendelea kuimarisha kituo cha Kilimo Anga kwa kukamilisha matengenezo ya ndege na taratibu za ununuzi wa ndege mpya moja ili kuondokana na utegemezi wa ndege za nje kwa ajili ya udhibiti wa visumbufu vya mazao.
“Hadi Aprili, 2023 Wizara imekamilisha matengenezo ya ndege ya kunyunyuzia viuatilifu iliyokuwa Nairobi nchini Kenya na taratibu za kuirejesha nchini zinaendelea. Vilevile, manunuzi ya ndege mpya kwa ajili ya shughuli za udhibiti wa visumbufu kwa njia ya anga yamefikia hatua ya tathmini ya kampuni tatu zilizoainishwa kwa ajili ya utengenezaji wa ndege maalum za udhibiti wa visumbufu”. Alisema Waziri Bashe.
Aidha, alifafanua kuwa imefika wakati kama nchi kujitegemea katika udhibiti wa nzige, kweleakwelea na visumbufu vingine vya milipuko kwa kutumia ndege zinazomilikiwa na nchi za unyunyuziaji badala ya kuendelea kutegemea ndege za mashirika ya nje.
Hatua hiyo ya Serikali inatajwa kusaidia udhibiti wa visumbufu katika mazao mara changamoto hiyo inapotokea na hivyo kuzuia hasara ambayo inaweza kujitokeza endapo hakutakuwa na hatua za haraka na ikiwa ni pamoja na matumizi ya ndege hizo maalum.