Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Samwel Warioba akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
HALMASHAURI ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imepanga kukutana na wadau wa madini 252 ili watekeleze takwa la kisheria la kuchangia maendeleo maeneo waliyowekeza.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Samwel Warioba ameyasema hayo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, baada ya kuulizwa swali la papo kwa hapo.
Warioba amesema watakutana na wadau wa madini ya Tanzanite 252 ili wapange utaratibu wa namna ya kuchangia maendeleo katika maeneo waliyowekeza.
Amesema ni wawekezaji wachache wanaoshiriki kuchangia maendeleo Simanjiro kama takwa la kisheria linavyotaka hivyo watafuatilia hilo ili litimizwe.
“Sisi kama Simanjiro mara nyingi tumekuwa hatupati mgao wa kuchangia maendeleo kwenye maeneo ya jamii kutoka kwa wawekezaji wa eneo kama sheria inavyoelekeza,” amesema Warioba.
Awali, diwani wa kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer aliuliza swali la papo kwa hapo kwenye baraza hilo juu ya idadi ya wawekezaji wanavyoshiriki kuchangia maendeleo Simanjiro.
“Ninahitaji kufahamu idadi ya wawekezaji wanavyoshiriki kuchangia maendeleo (CSR) kwenye maeneo yanayowazunguka kwenye wilaya ya Simanjiro.
Wachimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite Bilionea Saniniu Laizer na kampuni ya Franone Mining LTD ni miongoni mwa wadau wanaoshiriki kuchangia maendeleo Simanjiro.