Na John Walter-Manyara
Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mkoa wa Manyara limeiomba Serikali kuanza kuelekeza nguvu katika kuboresha maslahi yao kama ambavyo imekuwa ikifanya kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ombi hilo wamelitoa mjini Babati wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika kimkoa mjini hapa uwanja wa Kwaraa.
Katika risala yao wafanyakazi, wamesema kutokana na kupanda kwa gharama za maisha umefika muda sasa maslahi ya wafanyakazi yapewe kipaumbele.
“Kila siku hali ya maisha inapanda na kupelekea kila mashahara anapoupata mfanyakazi mwisho wa mwezi ndani ya wiki moja au mbili mshahara umekwisha na wiki zinazobaki ni amaisha ya tabu,dhiki na kuishi kwa kukopakopa” ilieleza risala ya TUCTA
Aidha TUCTA mkoa wa Manyara wamemuomba Rais kuboresha mishahara kwa kada zote pia ajira ziwe za staha na kuangalia uwezekano wa kuboresha maisha ya mfanyakazi hadi anapostaafu.
Akihutubia katika maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi mkoani humo kuhakikisha kuwa wanashughulikia changamoto za wafanyakazi badala ya kusuburi maadhimisho ya Mei Mosi.
Pia amesema maombi hayo atayawasilisha kwa mheshimiwa rais kama yalivyo.
Mkuu wa mkoa aliwataka waajiri kutoa mikataba ya ajira sambamba na stahiki nyingine kwa watumishi wao kama ambavyo, sheria za kazi zinavyoelekeza.
Amesema kuwa bado kuna changamoto ya waajiri wengi hususani katika sekta binafsi, kutotimiza wajibu wao kwa kutotoa mikataba ya ajira pamoja na stahiki nyingine kwa watumishi wao, jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kitaifa yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro Rais Samia alisema “Mishahara kwa mwaka huu mbali na upandishaji wa posho nilizosema tumejiandaa pia kupandisha madaraja, vyeo vitaendelea kupandishwa, kutenganisha makundi na madaraja mserereko wale ambao hawakupata mwaka jana watapata mwaka huu.
“Niseme pia kuna nyongeza za mishahara za mwaka ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zimesitishwa, nikaona kwa mwaka huu tuzirudishe kwa wafanyakazi wote kuna nyongeza za mishahara tunaanda na tutaendelea kama tulivyokuwa tunafanya zamani,” amesisitiza.
Rais Samia amesisitiza kuwa mwaka jana Serikali ilipandisha mishahara kwa asilimia 23.3 ambayo si kila mtu alifaidika ila lengo ilikuwa kuwainua wa kima cha chini na wengine wachache lakini kuna kindi kubwa halikuguswa.
Rais Samia amesema zipo taasisi ambazo zilishindwa kutekeleza agizo la kutoa nyongeza za posho kwa kuwa wakati anatoa agizo hilo bajeti ilikuwa imeshapita, kwa maana hiyo mavuno ya posho hizo yatakuwa kwenye bajeti ya mwaka huu, 2023/2024.
Amesema, mbali na upandishaji wa posho, mwaka huu pia ataendelea kupandisha madaraja, vyeo na madaraja mserereko upo mwaka huu.
“Kauli mbiu ya mwaka huu Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi, Wakati ni Sasa “