Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wakiwa kwenye Maadhimisho ya Sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambayo Kitaifa imefanyika Mkoani Morogoro Tarehe 01 Mei, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Profesa Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Dkt. Moses Kusiluka, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Tumaini Nyamhokya pamoja na Viongozi wengine wakiimba Wimbo wa Mshikamano (Solidarity) wakati wa Sherehe ya Mei Mosi ambazo Kitaifa zimefanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro tarehe 01 Mei, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono viongozi pamoja na Wafanyakazi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya kushiriki Maadhimisho ya Sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa zimefanyika Mkoani Morogoro tarehe 01 Mei, 2023.
Wafanyakazi kutoka Wizara, Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi wakiwa kwenye Maadhimisho ya Sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa yamefanyika Mkoani Morogoro tarehe 01 Mei, 2023.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Prof.Joyce Ndalichako, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan namna anavyowathamini wafanyakazi huku akimhakikishia kuendelea kuimarisha utatu ili kuwa na uhusiano mzuri mahala pa kazi.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi Kitaifa 2023 Mjini Morogoro, Waziri Ndalichako, amesema “Nikuhakikishie Mhe.Rais sisi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu itaendelea kuimarisha utatu kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa karibu na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Chama cha Waajiri na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili kudumisha na kuimarisha uhusiano mzuri mahala pa kazi na kuchochea ufanisi.”
Aidha, Mhe. Ndalichako amempongeza Rais Samia ndani ya miaka miwili ya uongozi wake kwa kuendelea kupandisha madaraja, nyongeza za mshahara, ongezeko la ajira mpya na ubadilishaji wa miundo ya madaraja kwa wafanyakazi nchini.
Amesema wafanyakazi wataendelea kumuunga mkono Rais Samia.
Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA), Tumaini Nyamhoka, amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kusimamia mahusiano mahala pa kazi.
Awali, akisoma risala ya TUCTA, Katibu Mkuu wa Shirikisho hiyo, Henry Mkunda, ameomba Serikali kuboresha kitengo cha Idara ya Kazi kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuongeza watumishi kwa kuwa waliopo ni wachache ili ajira za staha sipatikane kwa wafanyakazi.
“Tunakushukuru Mhe.Rais kwa kuondoa changamoto zote za ucheleweshaji wa mafao ya uzeeni na kukubali kutoa michango yao ya asilimia tano kwa wafanyakazi ambao waliondolewa kwa dosari kwenye vyeti,”amesema.
Mwenyekiti wa Chama Cha Waajiri nchini (ATE), Jayne Nyimbo, amemshukuru Waziri Ndalichako kwa ushirikiano anaoutoa katika utatu na kusisitiza uendelee ili kutatua changamoto za ajira kwa njia ya majadiliano.
Aidha, amesema waajiri wamekuwa wakitoa nafasi ya mafunzo tarajali kwa wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu na ufundi Stadi kupitia programu inayoratibiwa na Kitengo Cha Huduma za Ajira(Taesa) huku akitoa wito kwa waajiri kuendelea kutoa nafasi nyingi kwa wahitimu wajifunze na kuongeza ujuzi.