Wakuu wa Majeshi ya Polisi Nchi za jumuiya ya Afrika mashariki wamekutana kwa siku mbili Jijini Arusha na wametia saini makubaliano kadha ya mtangamano wa kufanyakazi kwa pamoja kupambana na makosa ya uhalifu unaovuka mipaka.
Akizungumza mara baada ya Utiliaji saini huo Mkuu wa jeshi la Polisi nchini (IGP)na mwenyeji wa Mkutano huo Simon Sirro ameeleza kuwa malengo ya kikao hicho cha siku mbili ilikuwa ni kujadili hali ya usalama na changamoto wanazokutana nazo wakati wa kukabiliana na uhalifu hususani maeneo ya Mipakani.
Amesema kuwa kuna makosa mbali mbali ambayo yamekuwa yakikinzana kisheria na Adhabu kwa nchini moja hivyo wameweka mkakati wa pamoja na ndio maana makubaliano hayo wanatia saini kuweza kujenga mtangamano imara kukabiliana kwa pamoja mapambano ya uhalifu kwenye ukanda wetu.
Amesema kuwa katika makubaliano hayo imeonekana ipo haja ya kuangalia maabara zetu kubwa zifanyekazi vipi kwa ushirikiano ili zienda na sheria moja ambayo itasaidia kuondoa changamoto za kimaabara ambazo kwa nchi moja ni kosa huku kwingine si makosa.
“Makosa yanayovuka mipaka yakiwemo Ujangili biashara ya binadamu madawa ya kulevya na Ugaidi haya ni makubaliano tuliowekeana leo kuna vitu tumekubaliana ndio maana tukasaini ili kujenga matangamano imara kwa lengo la kuweza kukabiliana na makosa hayo bila kupata vikwazo kutokana na sheria na adhabu ya nchi moja kukinzana na nyingine” alisema Sirro.
Kwa Upande wake Naibu katibu mkuu EAC anayeshughulikia Mtangamano wa shirikisho la Kisiasa Charles Njoroge amesema kuwa kikao hicho ni mkakati wa pamoja wa majeshi ya polisi katika nchi za Afrika mashariki kufikia kufanyakazi kwa pamoja kuondoa changamoto na kuongeza ufanisi katika kupambana na makosa yanayovuka mipaka.
Ameeleza kuwa ugadi makosa yanayovuka mipaka ikiwemo ujangili utakatishaji fedha haya yote yamejadiliwa kwa kina na ndio maana mmeona wametiliana saini makubaliano kadhaa kuweza kuondoa na kudhibiti uhalifu mipakani na ule unaovuka mikapa kwa ushirikiano.
Nae Naibu Mkuu wa jeshi la Polisi nchini Kenya Japhet Koome amesema kuwa kikao hicho kitasaidia nchi zetu kuona umuhimu wa sheria zetu kwenda kwa pamoja ili kuweza kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka na makosa ya kijinai ambayo sheria moja ya upande huu hailingani na upande ule.