Na Victor Masangu,Kibaha
Umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini wamempongeza mke wa Mbunge la Jimbo la Kibaha mji Selina Koka kwa kuweza kuwawezesha kiuchumi wanawake na kuwapatia mitaji ya fedha ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mji Elina Mgonja wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na wanawake pamoja na kuona uhai wa chama jinsi unavyokwenda.
Mgonja alisema kuwa Mama Koka ambaye pia ni mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha mji amekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na wanawake wenzake katika kuhakikisha analeta chachu ya maendeleo katika nyanja mbali mbali.
“Nipo katika ziara yangu katika kata mbali mbali lakini natoka kutoa shukrani zangu za dhati kwa mama Selina Koka kwa moyo wake wa kujitolea na kuwapatia mtaji wanawake kwa kuwapatia shilingi laki tano ili waweze kujikwamua,”alisema Mgonja.
Aidha Mwenyekiti huyo hakusita kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kwa kutekeleza ilani ya chama na kuchochea kasi ya maendeleo katika maeneo mbali mbali.
Kwa Upande wake Selina Koka aliwaomba wanawake wajasiriamali kujiunga katika makundi ili waweze kupatiwa mafunzo mbali mbali ambayo yatawasaidia katika kuendesha shughuli zao.
Pia Selina alitoa shukrani zake za dhati kwa Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuleta mabadiliko chanya katika kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo.
Nao baadhi ya wanawake wa UWT wamesema mitaji ya fedha ambayo wamewezeshwa na mlezi wao Selina Koka itaweza kuwa mkombozi kwao kutokana na kuondokana na wimbi la umasikini.