Na. Damian Kunambi, Njombe.
Katika kutekeleza agizo la Serikali lililozitaka Halmashauri mbalimbali kote nchini kuhakikisha kuwa kila mwaka zinapanda miti isiyopungua Ml. 1.5 ili kuwezesha utunzaji wa vyanzo vya maji Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kwa mwaka huu imeadhimia kupanda miti Ml. 7 ambapo miti Ml. 5 mpaka sasa tayari imekwisha pandwa ambayo ni sawa na asilimia 75 ya lengo la kazi hiyo.
Awali akisoma risala iliyoandaliwa na mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva mara baada ya kukamilisha mbio za mwenge mbele ya kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa katibu tawala wa wilaya ya Ludewa Daniel Ngalupela amesema kwa mwaka 2022 wilaya hiyo ililenga kupanda miti Ml.7 ambapo mpaka mwaka unaisha miti zaidi ya Ml.6 ilipandwa sawa na asilimia 86.12 ambapo katika idadi hiyo ya miti iliyopandwa miti zaidi ya Ml5.5 pekee ndiyo ilistawi ambayo ni sawa na asilimia 96.25.
Ngalupela ameongeza kuwa sambamba na shughuli hiyo ya upandaji miti lakini pia wilaya hiyo imeweza kutambua hifadhi ya vyanzo vya maji 267 ambavyo vimetambuliwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ambapo vyanzo 183 kati ya hivyo vilivyotambuliwa vimepandwa miti iliyo rafiki na maji huku wakizuia matumizi ya maeneo hayo kwa shughuli za kibinadamu.
“Vyanzo hivi vinahudumia wananchi wapatao 112,461 kati ya wananchi 151,361 wa wilayani hapa hivyo katika kuhakikisha vyanzo hivi vilivyopo katika misitu ya hifadhi yenye jumla ya ekari 61,075.51 kwa Wilaya nzima vinaendelea kutunzwa tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji mazingira ikiwemo kuchukua hatua dhidi ya uharibifu unaobainika kama uchomaji moto katika misitu” amesema Ngalupela.
Sanjali na kusomewa risala hiyo kiongozi wa mbio za mwenge Abdalla Shahib Kaim akiwa na jopo lake walipita na kukagua msitu wa hifadhi ya mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji wa Ihonjogolo uliopo katika kijiji cha Lufumbu kata ya Mlangali unaomilikiwa na halmashauri ya wilaya hiyo na kujionea vyanzo hivyo vya maji.
Kwa mujibu wa taarifa ya msitu huo imeeleza kuwa shughuli za kuhifadhi msitu huo pamoja na kuhifadhi chanzo cha maji umegharimu kiasi cha zaidi Ml. 20 kati ya hizo Ml 6 zilitumika kwa ajili ya kufanya mikutano ya uhamasishaji, kufanya tathmini ya rasilimali za msitu na kuandaa mpango wa usimamizi na sheria ndogo za utunzaji wa misitu huku zaidi ya Ml. 14 zikitumika kuboresha chanzo cha maji na kuboresha miundombinu ya maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tenki la maji.
Imeongeza kuwa umewezesha kujengwa kwa mtego wa maji ( intake) yanayotumiwa na wananchi wa kijiji cha Lufumbu, kitongoji cha Ihonjogolo chenye jumla ya wakazi 349 kitu ambacho kimepelekea wananchi wanao uzunguka msitu huo kuhamasika kuutunza msitu huo kwa kuweka mizinga 7 ya nyuki huku wakiendelea na uhamasishaji kwa wengine juu ya ufugaji huo.
Hata hivyo kiongozi wa mbio za mwenge huo Abdalla Shaib Hakim alipongeza utunzaji huo wa mazingira huku akisisitiza kuendelea kupanda miti ya kutosha pamoja kuhamasisha jamii katika kuvilinda vyanzo hivyo.
Aidha mwenge huo umepita katika miradi 8 ambayo ni vyumba viwili vya madarasa ya awali, Shamba la mikorosho lenye ekari 65, Zahanati katika kijiji cha Kimelembe, Jengo la utawala la Halmashauri, Kuzindua club ya wapinga rushwa shule ya sekondari Chief Kidulile, msitu wa asili unaotunza vyanzo vya maji pamoja na Lishe bora.