Kama mnavyofahamu kuna zoezi linaendelea la kusajili namba za simu kwa kutumia mfumo wa alama za vidole (Biometric) katika nchi nzima. Zoezi hilo kama lilivyotangazwa na kuelekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kila mmiliki wa namba ya simu atasajili namba yake kwa kwenda katika maduka na Mawakala wa kampuni za simu husika.
Katika siku za hivi karibuni kumejitokeza mtu/kikundi cha watu wanaosambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii unaowaelekeza watumiaji wa simu za mkononi kuwa wanaweza kujisajili kwa kutumia mfumo (Link) wanayoisambaza yenye jina la APPLICATION JISAJILI ONLINE BURE.
Wakati Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola vinafuatilia mtu au kikundi cha watu wanaosambaza ujumbe huo wa kupotosha umma, Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kwa wananchi wote kupuuza ujumbe huo na badala yake kila mmoja afuate maelekezo yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwani ndiyo sahihi na halali.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu kama huo katika kituo chochote cha Polisi kilichopo karibu au mamlaka zozote za kiserikali. Ikumbukwe jukumu la ulinzi na usalama ni letu sote Watanzania.