Tunapoelekea kipindi hiki cha kusherekea sikukuu ya Eid El Fitri Jeshi la  Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wananchi wote kuwa makini na  kusherekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu pasipo vitendo au viashiria  vyovyote vya uvunjifu wa amani 

Ikumbukwe kuwa wananchi wote katika Mkoa wa Mwanza wenye imani ya  kiislamu na hata madhehebu mengine kutumia muda huo kwenda kuabudu  pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya  starehe, wakati mwingine baadhi ya watu wasio wastaarabu wanaweza  kutumia kipindi hicho cha sikukuu kwa kufanya matukio ya uhalifu kutokana  na mikusanyiko ya watu maeneo mbalimbali. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linapenda kuwatoa hofu wananchi wa  Mkoa wa Mwanza na kuwahakikishia kwamba askari wake wamejipanga  kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wanasherekea sikukuu  za Eid El Fitr kwa amani na utulivu. Ulinzi utaimarishwa kwenye maeneo  yote ya kuabudia, viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya swala ya Iddi, fukwe  za ziwa, sehemu za starehe na maeneo mengine yote. Aidha, tunapenda  kuwatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa  makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa  madereva wa magari na pikipiki kuepuka kwenda mwendo kasi au kutumia  vilevi wakati wa kuendesha vyombo vya moto. 

Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi  hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu  

kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha  kwa kujaza watu kupita kiasi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza  tunawashukuru wale wote ambao tayari wamefunga kamera zao za CCTV katika maeneo ya starehe, hususani yale yanayokuwa na mikusanyiko ya  watu, yakiwemo maduka, hoteli, supermarket, malls, na maeneo ya benki.  Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunaendelea kuwasisitza wale  ambao hawajaweka kamera hizo, kuweka ili kuweza kubaini wahalifu na 

hata kurahisisha ukamataji endapo uharifu utatokea.  

Vilevile, wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto ili kuepuka  ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.  Hivyo jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza hatutaruhusu disko toto katika  maeneo mbalimbali badala yake wazazi wanashauiriwa kuwapeleka watoto  wao katika maeneo ya wazi ambapo kutakuwa na ulinzi na doria za  kutosha za askari wa Jeshi la Polisi tukishirikiana na vyombo vingine vya  ulinzi na usalama. 

Aidha, wananchi wachukue tahadhari za kutosha watokapotoka kwenye  makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na watoe taarifa kwa  majirani zao na pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu  wasikae kimya bali watoe taarifa haraka kwenye vituo vya Polisi vilivyo  karibu nao au kwa askari wetu wa doria, wanaofanya doria katika mitaa,  kwa wakuu wa polisi wa wilaya, maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi au  kwa Kmanda wa Polisi Mkoa ambaye namba zake za mawasiliano ni 0715- 009949 na 0739-009949. 

Jeshi la Polisi mkoa Wa Mwanza tunawatakia Eid Mubaraka wakazi wote  wa Mkoa wa Mwanza na tunawatakia washerekee sikukuu hizo kwa amani na utulivu.

Tarehe 16.04.2023 muda wa saa 21:45 usiku, huko maeneo ya Bwiru  Msikitini, kata ya Pasiansi, Tarafa na Wilaya ya Ilemela, kuliripotiwa taarifa  ya Emmanuel Nyambera, miaka 40, mfanyabiahashara na mkazi wa  Bwiru Msikitini aliyejipiga risasi kifuani upande wa kushoto na kupelekea  kifo chake. Emmanuel Nyambera alikuwa akimiliki Pistor yenye namba za  usajili TZCAR80190 Model namba 79 KCAL 38 aina ya charter ambayo  inauwezo wa kuchukua risasi tisa (9) na ndio aliyotumia kujifyatulia risasi  kifuani. 

Chanzo cha tukio hilo ni migogoro ya kifamilia iliyotokana na mgawanyo wa  mali za familia ambapo Emmanuel Nyambera alikua hajalidhia jambo  lililompelekea kuwa na msongo wa mawazo na kupelekea kujipiga risasi. Mwili wa Emmanuel umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu kwa  taratibu za mazishi. 

Jeshi la Polisi Mkoa Wa Mwanza linaendelea kutoa wito kwa wananchi  kutafuta njia nzuri na sahihi ya kutatua migogoro mbalimbali wanayokutana  nayo ilikuepusha madhara yanayoweza kujitokeza. 

Imetolewa na;- 

Wilbrod Mutafungwa – SACP. 

Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.