Na Mwandishi Wetu, MoHA, Zanzibar
HATIMAYE Fainali ya Michuano ya Kombe la Masauni na Jazeera Cup imefikia tamati ambapo yameibua Timu ya Mnazi Mmoja kuchukua zawadi ya Kitita cha Shilingi Milioni Mbili (2,000,000) pamoja na zawadi mbalimbali ikiwemo jezi na kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora.
Timu ya Kilimani ambayo imeshika nafasi ya pili imenyakua Shilingi Milioni Moja (1,000,000) kwenye Fainali hiyo iliyofanyika Alhamisi Usiku wa Aprili 20, 2023, katika Kiwanja cha Alabama, Jimbo la Kikwajuni, mjini Unguja, Zanzibar.
Zawadi hizo zimetolewa na Mgeni Rasmi wa Mashindano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Mohammed Said Dimwa, ambaye alitoa pongezi kwa Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo hilo kuendeleza michezo hiyo ambayo ni muhimu kwa afya na pia inaleta umoja.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye ndiyo Mbunge wa Jimbo hilo, Mhandisi Hamad Masauni alisema Mashindano hayo ni muhimu jimboni humo na yataendelea kufanyika kwa kuwa yanaleta umoja.
Pia aliwataka wazazi kuwafundisha maadili mema watoto pamoja na vijana wao ili kuepuka masuala ya ushoga kwa kuwa Mungu hapendi na hauwezi kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na jamii kwa ujumla.
Pia alitangaza kuwa, Uwanja huo uliofanyika fainali hiyo unatarajiwa kujengwa na kuwa wa kisasa ili kukuza vipaji vya michezo vya wananchi wa jimbo hilo.
Mashindano hayo ambayo ufanyika kila mwaka kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani yameandaliwa na Mbunge wa Jimbo hilo, Mhandisi Hamad Masauni ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.