Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 lililojengwa katika mradi wa maji Pambazuko uliotekelezwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa)kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 500 ambao umeanza kunufaisha wakazi wa mitaa miwili ya Mlete na Pambazuko.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,akiangalia mchoro wa mradi wa maji Pambazuko uliotekelezwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingiraManispaa ya Songea Souwasa,kushoto Mkuu wa wilaya ya Songea Wilman Ndile.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,akimpa cheti cha Heshima Akofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Doyasisi ya Ruvuma Raphael Haule kutokana na mchango wa kanisa hilo kutoa ardhi bure kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Mapambazuko,wa pili kulia Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki na wa pili kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Souwasa Mhandisi Patrick Kibasa.
Muhidin Amri,
Songea
WIZARA ya maji kupitia mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa),imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Pambazuko kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uvico-19.
Akitoa taarifa ya ujenzi kwa kiongozi
wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 Abdala Kaim, msimamizi wa ujenzi wa mradi huo Franki Tumbi alitaja fedha zilizotumika kutekeleza mradi huo ni zaidi ya Sh.milioni 578, zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Alisema,lengo kubwa la serikali kujenga mradi wa maji Pambazuko ni katika kutekeleza mkakati wake wa kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa mitaa miwili ya Pambazuko na Mlete yenye wakazi wapatao 3,990.
Aidha alisema,mradi huo utasaidia kuwapunguzia wananchi wa mitaa hiyo miwili muda wa kufuata huduma ya maji mbali na makazi yao na kushiriki vyema katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa mujibu wa Tumbi,vyanzo vya maji vya mardi huo ni visima viwili vyenye wa kuzalisha lita 518,400 kwa siku na mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 100.
Alisema,mamlaka inatekeleza kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuzingatia na kufuata sera ya maji ya mwaka 2002 ambayo inahakikisha huduma ya maji inapatikana na kumfikia mwananchi katika umbali usiozidi mita 400 kutoka katika makazi yake.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,amewapongeza wataalam wa Souwasa kwa usimamizi mzuri wa mradi huo ambao uliojengwa kwa ubora na unaendana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Amewataka wakazi wa mitaa hiyo ,kuhakikisha wanatunza mradi na miundombinu yake ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma ya maji.
Amewakumbusha juu ya wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na kutanguliza uzalendo pale wanapotekeleza miradi ya maji ili kwenda sambamba na adhima ya Serikali ya awamu ya sita ya kumtua mama ndoo kichwani.
Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Damas Ndumbaro amewakosoa baadhi ya watu wanaohoji kuhusu suala la serikali kukopa fedha kutoka mashirika mbalimbali Ulimwenguni ambapo ameeleza kuwa,fedha hizo zina manufaa makubwa kwa nchi na watanzania kwa ujumla.
Dkt Ndumbaro ambaye ni Waziri wa Sheria na Katiba alisema,fedha zilizokopwa na serikali ya awamu ya sita zimesaidia sana kutekeleza na kuboresha huduma za kijamii hapa nchini ikiwemo ujenzi wa mradi wa maji Pambazuko.
Amewaomba Watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao,kumuunga mkono Rais Dkt Samia katika jitihada zake za kuleta maendeleo na kuinua hali ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.
Mkazi wa mtaa wa Pambazuko Said Kajanja,ameishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umewasaidia kuondokana na changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama.
Alisema,kabla ya mradi huo walikuwa wanatumia maji ya visima vya asili na mito ambayo wakati wa masika hayakuwa safi na salama kwa kuwa yalichanganyika na uchafu mwingi.