Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 za maji lililojengwa katika mradi wa maji Muhuwesi na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru.
Meneja wa Ruwasa wilayani Tunduru Mhandisi Maua Mgala akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Muhuwesi kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdala Shaib Kaim(hayupo pichani) kabla ya kiongozi huyo kuweka jiwe la msingi.
Mhandisi wa maji kutoka ofisi ya meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Francis Maddal akionyesha mchoro wa mradi wa maji Muhuwesi wilayani humo uliotekelezwa kwa lengo la kuhudumia wakazi wa vijiji viwili vya Muhuwesi na Msagula.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Abdala Shaib Kaim,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Muhuwesi wilayani Tunduru Neema Komba kulia,baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi huo.
Meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa)mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga kulia,akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu kushoto,wakati wa uwekezaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji Muhuwesi wilayani Tunduru.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
KIONGOZI wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa 2023 Abdalla Shaib Kaim,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa jitihada inazofanya za kuimarisha na kuboresha sekta ya afya hapa nchini.
Kaim ametoa pongezi hizo jana,wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la huduma za dharura katika Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma.
Alisema tangu serikali ya awamu ya sita iingie madarakani miaka miwili iliyopita, imeonyesha kwa vitendo dhamira ya kuwatumikia Watanzania hususani wananchi wa kawaida kwa kuwaondolea changamoto mbalimbali zilizokuwepo kwa muda mrefu ikiwemo huduma bora za afya.
Alisema, lengo la serikali kujenga jengo hilo ni kuhakikisha hakuna mwananchi anaweza kupoteza maisha kwa kukosa huduma za matibabu na kutoa wito kwa wakazi wa wilaya ya Tunduru kuwa na mazoea ya kwenda na kutumia vituo vya kutolea huduma vilivyopo katika maeneo yao kwa ajili ya kupata matibabu.
Amewaagiza vongozi wa wilaya
ya Tunduru,kukamilisha ujenzi wa jengo hilo haraka ili wananchi waanze kupata huduma na kufaidi matunda ya Serikali yao badala ya kuchukua muda mrefu.
“haya ni matunda yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,katika kuimarisha sekta ya afya hapa nchini”alisema Kaim.
Aidha,amemwagiza Mganga Mkuu wa wilaya hiyo kutoa mafunzo kwa watumishi watakaofanya kazi katika jengo hilo ili wawe na ujuzi zaidi wa kutumia vifaa vitakavyofungwa na namna ya kuwahudumia wagonjwa watakaoletwa kupata matibabu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Athuman Mkonoumo alisema,ujenzi wa jengo hilo unatekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 369,683,004.10 kati ya hizo Sh.milioni 300 zimetolewa na Serikali huku Sh.milioni 69,683,004.10 ni mapato ya ndani ya Halmashauri.
Alisema,jengo hilo linajengwa kwa mfumo wa Force Akaunti na ujenzi wake ulianza rasmi mwezi Februari na ulitarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka jana,lakini kutokana na changamoto mbalimbali mradi haukuweza kukamilika kwa muda uliopangwa.
Dkt Mkonoumo alisema, kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 98 na kazi zilizosalia ni ukamilishaji wa ufungaji wa viyoyozi, na uwekezaji wa mfumo wa hewa tiba utakaowekwa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi.
Alieleza kuwa,kukamilika kwa mradi huo kutasaidia sana utekelezaji wa azma ya Serikali ya kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake hasa ikizingatiwa kuwa wilaya ya Tunduru ni kubwa kwa eneo na ina idadi ya watu wapatao 412,054.
Alisema,mradi huo utawezesha kupunguza rufaa za matibabu kwa wagonjwa na kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wanaostahili kupata rufaa kwenda Hospitali nyingine nje ya wilaya ya Tunduru.