Naibu Waziri, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Aprili 13,2023 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mwendendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Aprili 2023.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Uwekezaji Viwanda na Biashara imetoa mwendendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa Mwezi Aprili 2023, huku,mchele,mahindi,unga wa mahindi,maharage vikipungua bei na vifaa vya ujenzi vikiendelea kuonesha uhimilivu kwa kutokuwa na mabadiliko.
Pia imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa muhimu nchini hasa katika kipindi hiki cha Mfungo Mtukufu wa Ramadhan.
Hao yameelezwa leo Alhamisi Aprili 13,2023 jijini Dodoma ,na Naibu Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara,Exaud Kigahe wakati akiwasilisha taarifa ya mwendendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Aprili 2023.
Mahindi yapungua bei
Mhe. Kigahe amesema bei ya mahindi kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 800 na 1,650 kwa kilo.
Amesema bei ya juu ya mahindi imepanda kwa asilimia 1.5 ambayo ni sawa na ongezeko la Shilingi 25 kwa kilo, wakati bei ya chini imepungua kwa asilimia 5.9 sawa na punguzo la Shilingi 50 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi, 2023 ambayo ilikuwa kati ya Shilingi 850 na1,625 kwa kilo.
“Bei za chini zipo katika Mikoa ya Ruvuma na Iringa na bei ya juuimeonekana katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara,”amesema Mhe. Kigahe
Amesema uchambuzi unaonesha kuwa wastani wa bei ya mahindi kwa mwezi Aprili 2023 imepungua kwa asilimia 0.8 ukilinganisha na wastani wa bei ya mwezi Machi 2023.
“Kupungua huko kumesababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo kumekuwa na uhakika wa mavuno ya mahindi kwa wakulima wengi, hali ambayo imesababisha wakulima kuachilia akiba waliohifadhi ili kupisha nafasi kwa ajili ya mavuno ambayo yanatarajiwa hivi karibuni,”amesema Mhe. Kigahe
Unga wa Mahindi
Aidha amesema bei ya Unga wa mahindi kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 1,200 na 2,100 kwa kilo.
Amesema bei ya juu ya unga wa mahindi imeshuka kwa asilimia 20.0 sawa na kupungua kwa shilingi 75 kwa kilo, wakati bei ya chini ya unga wa mahindi imeshuka kwa asilimia 20 sawa na kupungua kwa Shilingi 300 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa ni kati ya Shilingi 1,500 na 2,175 kwa kilo.
Mhe. Kigaheamesema bei ya chini ipo katika Mikoa ya Iringa, Tabora na Songwe na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Pwani, Lindi, Mara na Dar es Salaam.
“Uchambuzi unaonesha kuwa wastani wa bei ya Unga wa Mahindi kwa mwezi Aprili 2023 imepungua kwa kati ya asilimia 2.1 ukilinganisha na wastani wa bei ya mwezi Machi 2023.
“Upungufu huo wa wastani wa bei umesababishwa na kushuka kwa wastani wa bei ya mahindi ambayo ndiyo malighafi kubwa inayozalisha Unga wa Mahindi,”amesema Mhe. Kigahe
Mchele
Kwenye Mchele Kigahe amesema kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 2,350 na 3,500 kwa kilo.
Amesema bei ya juu ya mchele imeshuka kwa asilimia 2.8 sawa na pungufu ya shilingi 100 kwa kilo, wakati bei ya chini ya mchele imeshuka kwa asilimia 13 sawa na pungufu ya shilingi 350 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa ni kati ya Shilingi 2,700 na 3,600 kwa kilo.
Amesema Mikoa yenye bei ya chini ni Katavi, Tabora na Mwanza na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Pwani, Kagera na Mtwara.
Maharage
Kigahe amesema bei ya maharage kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 2,175 na 3,800 kwa kilo.
Amesema bei ya juu ya maharage haijabadilika, wakati bei ya chini imeshuka kwa asilimia 27.2 sawa na pungufu ya shilingi 813 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa kati ya Shilingi 2,988 na 3,000 kwa kilo.
Amesema bei ya chini inapatikana katika Mikoa ya Ruvuma, Katavi na Songwe na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Manyara, Pwani na Kilimanjaro.
Amesema uchambuzi unaonesha kuwa wastani wa bei ya maharage kwa mwezi Aprili 2023 imepungua kwa asilimia 7.0 ukilinganisha na bei ya wastani ya mwezi Machi 2023.
“Maharage ni mojawapo ya mazao ambayo yameanza kutoa mavuno na kuingia sokoni na hivyo kusababisha wastani wa bei ya zao hilo kushuka,”amesema Kigahe.
Viazi Mviringo
Naibu Waziri huyo amesema bei ya Viazi Mviringo kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 900 na 1,800 kwa kilo.
Amesema bei ya juu imeshuka kwa asilimia 10 sawa na shilingi 200 kwa kilo, wakati bei ya chini imepanda kwa asilimia 1.4 sawa na ongezeko la Shilingi 12 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa kati ya Shilingi 888 na 3,000 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa ni kati ya Shilingi 888 na 2,000 kwa kilo,”Amesema
Amesema bei ya chini ipo katika Mikoa ya Singida, Tabora, Geita na Iringa na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Rukwa, Songwe na Pwani.
Amesema uchambuzi unaonesha kuwa wastani wa bei ya Viazi Mviringo kwa mwezi Aprili 2023 imepungua kwa asilimia 2.7 ukilinganisha na wastani wa bei ya mwezi Machi 2023.
Unga wa Ngano
Amesema bei ya unga wa ngano kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 2,000 na 2,400 kwa kilo.
Mhe. Kigahe amesema bei ya juu na ya chini ya unga wa ngano imepanda kwa asilimia 4.3 na 11.1 sawa na ongezeko la Shilingi 100 na 200 kwa kilo mtawalia ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwani kati ya Shilingi 1,800 na 2,300 kwa kilo.
Amesema Bei ya chini ipo katika Mikoa tisa (9) nchini na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Songwe, Mbeya na Singida.
Sukari
Kigahe amesema Bei ya sukari kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 2,650 na 3,300 kwa kilo.
Amesema Bei ya juu ya sukari imepanda kwa asilimia 5.6 sawa na ongezeko la Shilingi 175 kwa kilo, wakati bei ya chini imepungua kwa asilimia1.9 sawa na Shilingi 150 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi ambayo ilikuwa ni kati ya Shilingi 2,700 na 3,125 kwa kilo.
Amesema bei ya chiniipo katika Mikoa ya Tanga, Singida, Songwe na Manyara na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Ruvuma, Geita, Iringa, Pwani na Rukwa.
Mafuta ya Kupikia
Amesema bei ya mafuta ya kupikia ya Alizeti kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 4,000 na 8,500 kwa lita.
Vile vile, bei ya mafuta ya kupikia ya Mawese (Korie na Safi) ni kati ya Shilingi 3,500 na 7,250 kwa lita.
Amesema Bei ya chini ya mafuta ya kupikia ya Alizeti imeshuka kwa asilimia 11.1 sawa na shilingi 500 ikilinganishwa na mwezi Machi, 2023 ambayo ilikuwaShilingi 4,500.
Vilevile, bei ya chini ya mafuta ya Mawese (korie na safi) imeshuka kwa asilimia 22.2 sawa na Shilingi 1,000 ikilinganishwa na mwezi Machi, 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 4,500 kwa lita.
Amesema Bei ya chini ya mafuta ya kupikia ya Alizeti ipo katika Mikoa ya Singida, Iringa na Manyara na bei ya juu ipo katika Mikoa Pwani, Mtwara na Lindi.
Vifaa vya ujenzi
Amesema bei ya saruji (42.5) kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 14,650 na 24,500 kwa mfuko wa kilo 50.
Amesema bei hiyo imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023.
Amesema Mikoa yenye bei ya chini ni Tanga, Dar es Salaam na Mtwara na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Mara.
Amesema bei ya nondo mm 10 kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 16,000 na 23,500 amedai bei ya juu imepanda kwa asilimia 6.8 sawa na shilingi 1,500 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 22,000.
Kigahe amesema Bei za chini zipo katika Mikoa ya Dodoma, Tanga na Arusha na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Songwe, Ruvuma, Iringa, Manyara na Rukwa.
Amesema Bei ya nondo mm 12 kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 22,000 na 28,000 ambapo Bei ya chini imepanda kwa asilimia 15.7 sawa na shilingi 3,000 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 19,000.
Kwenye bati amesema bati nyeupe geji 30 kwa mwezi Aprili ni kati ya Shilingi 21,500 na 30,000 ambapo Bei ya juu ya bati imepanda kwa asilimia 9.1 sawa na shilingi 2,500 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi, 2023 ambayo ilikuwa Shilingi 27,500.
Amesema Bei ya chini ipo katika Mikoa ya Dodoma, Songwe na Kigoma na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Tabora.
Kwa ujumla, wastani wa bei ya vifaa vya ujenzi (Nondo, Saruji na Mabati) imeendelea kuonesha uhimilivu kwa kutokuwa na mabadilliko ambayo yapo kwenye digiti moja, kitu kinaochoonesha kuhimili mfumoko wa bei.
“Wastani wa bei ya saruji aina ya 42.5 na ile ya aina ya 32.5 kwa mwezi Aprili 2023 imepungua kwa asilimia 1.1 na 2.0 mtawalia ukilinganisha na wastani wa bei ya saruji ya aina hiyo hiyo kwa mwezi Machi 2023.
Amesema hali hiyo inaweza kuwa imechangiwa na ongezeko la uzalishaji katika viwanda vya ndani vya kuzalisha saruji.
Vilevile, wastani wa bei ya mabati ya Geji 32, Geji 30 na Geji 28 kwa mwezi Aprili 2023 imepanda kwa asilimia 2.8, 1.7 na 1.4 mtawalia ukilinganisha na wastani wa bei ya mwezi Machi 2023.
Aidha, wastani wa bei ya Nondo za mm 10, mm 12, na mm 16 kwa mwezi Aprili 2023 imepanda kwa asilimia 3.0, 0.8 na 3.0 mtawalia ukilinganisha na wastani wa bei za mwezi Machi 2023.
Kupanda kwa bei kwa bidhaa za nondo na mabati kunaweza kuwa kumesababishwa na kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa hizo kwa watumiaji.
Katika hatua nyingine,Naibu Waziri huyo amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti ongezeko la bei zabidhaa muhimu nchini hasa katika kipindi hiki cha Mfungo Mtukufu wa mwezi wa Ramadhani.