Na Mwandishi wetu, Mbulu
MBUNGE wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Regina Ndege amepiga vita mmomonyoko wa maadili na kuwaasa wazazi na walezi nchini, kusimamia maadili ya watoto wao ili kuwa na jamii bora kwa Taifa la kesho.
Ndege ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Dotina, Kata ya Hayderere Wilayani Mbulu Mkoani Manyara.
Amesema hivi sasa katika maeneo mbalimbali nchini kumekuwepo na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa watoto hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuchukua hatua.
“Hivi sasa kwenye maeneo tofauti tofauti hapa nchini kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili na bila wazazi na walezi kuchukua hatua za kukomesha hayo, jamii ya miaka ijayo itakuwa na tatizo,” amesema mbunge Ndege.
Amesema matukio ya ubakaji, ulawiti kwa watoto na ndoa za utotoni ni janga ambalo pia linawakumba watoto hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuchukua hatua kwenye hayo.
“Wazazi ni sehemu ya watoto wetu kuweza kufanya vizuri hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kusimamia na kufuatilia mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani hata mashuleni,” amesema mbunge Ndege.
Amesema kutokana na wazazi na walezi kuchukua hatua kwenye malezi yao kutawajengea uwezo watoto katika misingi imara na maadili mema yanayofuata mila na desturi za watanzania.