Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (kushoto) na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko wakati wa makabidhiano ya msaada wa vifaa tiba katika Kituo cha Afya Sungusungu.
Shehena ya baadhi ya vifaa hivyo muda mfupi kabla ya kukabidhiwa
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko (kushoto) akisaini nyaraka za makabidhiano ya vifaa hivyo. Kulia ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara akiongea katika hafla hiyo
Wageni waalikwa wakiangalia jinsi vifaa hivyo vinavyofanya kazi
Viongozi mbalimbali wa Wananchi pia walihudhuria hafla hiyo
*****
MGODI wa Dhahabu wa Barrick North Mara na wakandarasi wake mgodini wamekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 120 katika Kituo cha Afya Sungusungu kilichopo Nyamongo wilayani Tarime.
Hafla ya kukabidhi msaada huo imefanyika katika kituo hicho na kuhudhuriwa na wafanyakazi wa mgodi,wawakilishi kutoka makampuni yanayofanya kazi katika mgodi,viongozi wa Serikali wilayani Tarime na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mh. Mwita Waitara
Akiongea wakati wa hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Apolinary Lyambiko, amesema kampuni imeshirikiana na wakandarasi wake kuchanga shilingi dola 59,587.60 kwa ajili ya ununuzi na ufungaji wa vifaa hivyo.
“Desemba mwaka jana mimi na wafanyakazi wenzangu tulitembelea kituo hiki na kujionea mapungufu ya vifaa tiba. Kwa kuzingatia umuhimu wa kituo hiki katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na wafanyakazi wa mgodi, Januari 2023 niliagiza idara yetu ya Mahusiano na ile ya Afya kuandaa kikao na wakandarasi wanaofanya kazi mgodini ili kwa pamoja tuone namna tunavyoweza kuchangia manunuzi wa vifaa tiba,” amesema Lyambiko.
Amesema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa vitasaidia kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya zikiwemo za mama na mtoto katika kituo hicho, na kwamba msaada huo ni sehemu ya uwajibikaji wa mgodi wa North Mara na wakandarasi hao kwa jamii inayouzunguka.
“Malengo ya mgodi ni kuendelea kushirikiana na wakandarasi wote kama wadau muhimu katika kutekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka ili kuimarisha mahusiano na mshikamano,” amesema Lyambiko.
Baadhi ya Kampuni za wakandarasi zilizoshirikiana na mgodi kufanikisha msaada huu ni pamoja na Kemanyanki, RES, Wings, Boart Longyear, AKO na PKM.
Akipokea na kukabidhi vifaa tiba hivyo kwa uongozi wa Kituo cha Afya Sungusungu na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameushukuru mgodi wa North Mara na wakandarasi hao, akisema wameweka alama nzuri katika eneo hilo.
“Haya yote ni matunda ya mahusiano na ushirikishwaji,” amesema Mbunge Waitara na kuahidi kuandika barua ya kuushukuru Mgodi na wakandarasi hao kutokana na msaada huo wa vifaa tiba.
Mbunge Waitara ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba wadau hao wa maendeleo kuangalia uwezekano kutoa msaada wa ujenzi wa majengo ya huduma za upasuaji na za mama na mtoto katika kituo hicho.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Sylvanus Gwiboha, ameshukuru na kusema msaada huo una maana kubwa katika utoaji wa huduma bora za afya.
“Afya bora haiwezi kupatikana kama hakuna vifaa tiba bora. Ninaamini Mungu atawabariki kwa kazi hii nzuri. Vifaa mlivyotoa vitawapunguzia wananchi gharama za kusafiri kwenda wilayani kutafuta huduma za vipimo vya afya”,amesema.
Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Malema Soro amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuhakikisha mgodi wa North Mara na wadau wote wa maendeleo katika eneo hilo hawabughudhiwi katika utekelezaji wa shughuli zao.
“Viongozi tusimamie wadau hawa wasibughudhiwe katika kazi zao maana wakizalisha zaidi watatoa kitu kikubwa zaidi kwa jamii. Hapa wamemsaidia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutupatia vifaa tiba ambavyo vinakwenda kusaidia wananchi wetu,” amesema Malema.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba hivyo ni pamoja na Diwani wa Viti Maalum, Felister Range na wenyeviti wa vijiji, Paul Bageni (Mjini-Kati) na Mwita Msegi (Nyangoto).
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.