WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa TFS Kanda ya Mashirika mara baada ya uzinduzi wa Kampeni ya Aprili ya Kijani mkoani Morogoro.
Mkuu wa kitengo cha Habari TFS Kanda ya Mashariki Suleiman Burenga akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kampeni ya April ya kijani mkoani Morogoro.
NA FARIDA MANGUBE MOROGORO.
WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk. Selemani Jafo amezitaka taasisi zinazojusika na uhifadhi wa mazingira kushirikisha jamii katika utunzaji wa miti inayopandwa maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Jafo amesema hayo mkoani Morogoro wakati akizindua kampeni ya Aprili ya kijani ilioandaliwa na Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mlimakola Dayosisi ya Morogoro.
Amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wadau wa uhifadhi hasa wanaondesha kampeni za kupanda miti katika maeneo mbalimbali lakini changamoto ni usimamizi mdogo kwenye utunzaji kuhakikisha miti hiyo inakuwa
Ameongeza kusema kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi zinaonekana dhahili kwani kumekuwa na mvua zisizo tabirika, ukame na kuathili uzalishaji kenywe sekta ya kilimo na Mifugo na kuepelekea kuporomoka kwa uchumi wa nchi.
“Kukosekana kwa mvua katika maeneo mengi ya nchi kunakosababisha bei za mazao kuwa juu na kuleta njaa kwa nchi ambapo jamii inapaswa kuzitafakari kwa kina athari hizo na kuacha kukata miti hovyo na kuchoma moto usio na faida ili kutunza misitu iliyopo kwa manufaa ya nchi na wananchi kwa ujumla.” Alisema Jafo.
Awali Askofu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro Jacob Ole-Mameo aliitaka jamii kutambua kuwa uharibifu wa mazingira ni jambo linalochangia mwanadamu kupoteza uhai wake kwa asilimia kubwa kwa sababu mazingira yanapoharibika mwanadamu atakosa mahitaji muhimu ikiwemo maji, hewa nzuri na chakula na hivyo kutishia uhai wao.
Naye Mwakilishi wa Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kanda ya mashariki Suleiman Burenga alihimiza jamii kujenga tabia ya kuitunza miti inayopandwa kila mara kwa manufaa yao na nchi nzima kwa ujumla.
Alisema upandaji wa miti ni kitu muhimu kwa sababu unasaidia kuiepusha jamii kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ambapo TFS imetoa miche takribani 2000 itakayopandwa kwenye jimbo la Morogoro.