Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck akiwakabidhi mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo, mwenyekiti wa Halmashauri ya Nachingwea Adinani Mpyagila na afisa elimu sekondari Endrew Muhulo wakati siku ya utoaji tuzo kwa waliofanya vizuri kwenye sekta ya elimu
Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck akiwakabidhi mkuu wa wilaya ya Nachingwea Mohamed Hassan Moyo, mwenyekiti wa Halmashauri ya Nachingwea Adinani Mpyagila na afisa elimu sekondari Endrew Muhulo wakati siku ya utoaji tuzo kwa waliofanya vizuri kwenye sekta ya elimu
Na Fredy Mgunda, Lindi.
MKOA wa Lindi umeendelea kufanya vizuri kwenye sekta ya elimu kwa kufaulisha wanafunzi kwa miaka mitatu mfululizo kwa asilimia 100 na kuongeza ufaulu wa kimadaraja jambo ambalo linasaidia watoto wengi kupata elimu.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa elimu, uzinduzi wa mpango mkakati wa elimu 2023 na sherehe za utoaji wa tuzo za ufaulu wa mitihani na pimaji za mwaka 2022/2023, Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck alisema kuwa ufaulu wa kidato cha nne katika kipindi cha miaka miwili mfululizo (2021-2022), mkoa wetu umeendelea kufaulisha wanafunzi wake wote kwa 100%. Kwa upande wa ufaulu kimadaraja, mkoa umeongeza idadi ya Wanafunzi wanaopata daraja la kwanza kutoka 426 mwaka 2021hadi 645 mwaka 2022 (sawa na ongezeko la 33.95%), Daraja -l kutoka wanafunzi 1,055 mwaka 2021 hadi 1,283 mwaka 2022 (sawa na ongezeko la 17.77%) na kupunguza daraja la IV kutoka wanafunzi 4 mwaka hadi 1 mwaka 2022 (sawa na punguzo la 75%).
Taleck alisema kuwa katika mtihani wa kidato cha sita mkoa huo umeendelea kupandisha ufaulu kutoka 92.51l% mwaka 2021 hadi 95.52% mwka 2022 ikiwa ni ongezeko 3.02%.
Kwa upande wa madaraja ya ufaulu mkoa wa Lindi umeongeza Wanafunzi wanaopata Daraja la |-|| kutoka 2,352 mwaka 2021 hadi 2,612 mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la 11.05% na kupunguza daraja la sifuri kutoka wanafunzi 539 mwaka 2021 hadi 334 mwaka 2022 sawa na punguz0 la
38.03%.
Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck alisema kuwa Halmashauri ya Liwale imefanikiwa kupunguza wanafunzi wanaopata daraja sifuri kutoka Wanafunzi 14 (2021) hadi wanafunzi 2 (2022) tu ndani ya wilaya.
Aidha Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Taleck aliwataka wazazi kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi waweze kupata chakula wakiwa shuleni kwa lengo la kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule zote za mkoa wa Lindi.
Alisema kuwa wanafunzi wasipotapa chakula shuleni hawawezi kufanya vizuri kimasoma kutokana na kila wakati kukabiliana na njaa wawapo darasani na kuwaondolea umakini wa kufuatilia masomo darasani.
Taleck aliwataka viongozi,walimu na wazazi kukemea kwa dhati vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa jamii ili kuwawezesha wanafunzi kusoma na kupata wananchi wengi ambao wamesoma katika mkoa wa Lindi.
Mkoa wa Lindi umeendelea kupandisha ufaulu kutoka 86.32% mwaka 2021 hadi 86.42% mwaka hii ikiwa ni ongezeko la 0.10% huku Baraza la Mitihani la Tanzania iliyotolewa kwa mwaka 2020 na 2021, imeutaja Mkoa wa Lindi Kuwa miongoni mwa Mikoa mitatu iliyofanikiwa kupandisha ufaulu kwa miaka mitatu mfululizo.
Awali akisoma taarifa kwa mgeni rasmi, afisa elimu mkoa wa Lindi Joseph Mabeyo alisema kuwa kufikia 31 Januari, 2023, Mkoa ulikuwa na Walimu wa Shule za Msingi 3,500 kati ya Walimu 5,450 wanaohitajika na upungufu wa walimu 1,950 sawa na asilimia 35.78 na kwa upande sekondari mkoa una walimu 1,701 kati ya walimu 1,950 wanaohitajika na upungufu wa walimu 249 sawa na asilimia 12.77.