Na. Tamimu Mbegu – Polisi Makao Makuu.
Jeshi la Polisi nchini litaendelea kushirikiana na wananchi na waumini wa dini zote katika kuimarisha usalama wa maisha na mali ikiwemo kubaini na kutanzua uhalifu wa kijinai pamoja na ajali za barabarani katika kuelekea ibada za sherehe za sikukuu ya Pasaka na muendelezo wa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani.
Hayo yalisemwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime makao makuu ya Polisi jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo habari kuhusu tahadhari kuelekea sikukuu ya Pasaka.
Misime alisema kuwa jeshi la polisi nchini katika mikoa na vikosi vyote limejipanga kikamilifu katika kuimarisha doria maeneo ya ibada na kwenye viwanja vya starehe kuhakikisha kwamba sherehe hizo zinasherekewa kwa amani na utulivu.
“Jambo kubwa ni kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake katika kuimarisha usalama wa raia na mali.” alisema Misime.
Aidha, alitoa rai kwa viongozi wa nyumba za ibada ambazo zitakuwa na ratiba za ibada kuimarisha kamati za ulinzi na kuwasiliana na wakuu wa polisi wa maeneo yao ili waweze kujadili namna ya kuimarisha ulinzi na usalama wakati wa ibada hizo.
Vilevile amewataka Wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao kwa kuangalia na kutambua maeneo yote watakayokuwa wanasheherekea sikukuu ili wasiweze kupata madhara ya aina yoyote ikiwemo kupotea wakati wa pasaka.
Jeshi la Polisi litaendelea na mkakati wake wa kuelimisha wananchi ili waweze kuwa na ushirikiano na Jeshi la Polisi kwa kuwa ushirikiano huo ndio silaha kubwa katika kubaini na kuzuia uhalifu.