Na Victor Masangu,Kibaha
Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kibaha mji Ramadhani Kazembe amewataka vijana wenzake kuhakikisha wanashikamana kwa pamoja na kutimiza wajibu wao ipasavyo kwa kuchapa kazi kwa uzalendo ili kuleta chachu ya maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake katika kata ya Tangini yenye lengo la kuweza kuzungumza na vijana pamoja na kutoa shukrani zake za dhati kwa kuweza kumchagua kushika nafasi hiyo ya Mwenyekiti.
Mwenyekiti huyo alisema kwa sasa suala la uchaguzi limeshamalizika hivyo hakuna budi kuachana kabisa na makundi na kuelekeza nguvu zao zote katika kuweka misingi imara kuanzia ngazi za matawi hadi ngazi ya Wilaya ikiwa sambamba na kutenda haki.
Aidha katika hatua nyingine Mwenyekiti Kazembe amesema lengo lake kubwa ni kuendelea kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo kwa kushirikiana na vijana wenzake ili kuweza kuleta chachu ya maendeleo katika jumuiya ya vijana.
Pia alifafanua kwamba ataendelea kuwatumikia na kuwaongoza kikamilifu vijana wenzake katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi kwa kuzingatia kanuni ya umoja wa vijana Kama inavyoelekeza katika ibara ya saba na nane kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi.
Kwa upande wake Katibu wa Uvccm Kibaha mji Gamalu Makona amesema kwamba ataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wenzake pamoja na vijana ili kuweza kuimarisha jumuiya ya umoja wa vijana.
Ziara ya Mwenyekiti wa Uvccm Wilaya ya Kibaha mjini katika kata ya Tangini imeweza kuleta tija zaidi kwa jumuiya hiyo kutokana na kujadili Mambo mbali mbali kwa maslahi mapana ya vijana pamoja na jamii kwa ujumla.