Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akihutibia wananchi wa kata ya Nyasaka katika viwanja vya Mkombozi
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akikagua barabara ya kutoka Msuka kuja Kiloleli B
Afisa Tarafa wa wilaya ya Ilemela Ndugu Godfrey Mzava akizungumza na wananchi wa mtaa wa Kiloleli B kata ya Nyasaka katika viwanja vya Mkombozi
Kiasi cha shilingi bilioni nne na milioni mia sita na kumi zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe Samia Suluhu Hasan kwa wilaya ya Ilemela katika sekta ya Ardhi kwaajili ya kupanga na kupima viwanja lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia ardhi yao
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake katika kata ya Nyasaka viwanja vya Mkombozi ambapo amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya Mhe Rais Samia Jimbo lake limepata bilioni mbili na milioni mia mbili hamsini katika sekta ya afya, Bilioni Moja na milioni sitini kwa elimu msingi na Bilioni Tano na milioni 250 kwa elimu sekondari
‘… Katika kipindi chake cha miaka miwili Rais Mhe Samia ametutendea makubwa sana, Tumshukuru na tuendelee kumuombea kwani Ilemela tumepewa fedha nyingi za maendeleo ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula mbali na kuwaasa vijana kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri amekemea vitendo vya unyanyasaji na ukatili vinavyoendelea katika jamii pamoja na kuwaasa wananchi kuripoti polisi kila vinapojitokeza vitendo hivyo
Akimkaribisha Mbunge huyo, Afisa tarafa wa wilaya ya Ilemela Ndugu Godfrey Mzava amempongeza Mbunge huyo kwa juhudi zake katika kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao na kwamba Serikali ya wilaya iko pamoja nae
Nae mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela, Afisa Maendeleo wa manispaa hiyo Ndugu Sitta Singibala amewaasa wananchi kutumia mikutano ya hadhara kwaajili ya kunufaika na mfuko wa maendeleo ya jamii wa kuhudumia kaya masikini TASAF kwa wale wenye sifa
Abdulrahman Simba ni diwani wa kata ya Nyasaka, Amemshukuru Mbunge Dkt Mabula na kuipongeza Serikali kwa kuleta zaidi ya milioni mia Tano ndani ya kata yake kwaajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo
Mbunge Dkt Angeline Mabula yupo ziara jimboni kwaajili ya kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza kero, pongezi, ushauri na changamoto za wananchi