Na Lucas Raphael,Tabora
Jeshi la polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora limewakamata watU 13 akiwemo Mtemi wa jeshi la jadi Sungu-sungu na kuwafikisha katika mahakama ya hakimu mfawidhi wilaya ya Igunga kwa tuhuma ya mauaji ya wafugaji watatu wa kata ya Isakamaliwa wilayani Igunga.
Mwendesha mashitaka wa Polisi wilaya ya Igunga Elimajidi Kweyamba leo aliwataja majina washitakiwa mbele ya hakimu wa wilaya ya Igunga Ridia Ilunda ambapo alisema mshitakiwa wa kwanza Jijadi Katambi (43) ambae ni mtemi wa jeshi la Jadi Sungu-sungu kata ya Isakamaliwa.
Watu wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni Maleba-Machenge (37) Ngoga Ifegelo (50) Ndulu-Manyenye (32) Shakali-Ifegelo (30) Magembe-Mwandu (25) Mahona-Jilala (35) Bakari Hamis (45) Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha isakamaliwa Shija Mboje (48) na Mwalimu wa shule ya msingi Isakamaliwa Michael Masanja (36).
Wengine ni Kulala-Shigela (38) Masunga-Kulwa (39) na Nkwabi-Mipawa (58) wote wakazi wa kata ya Isakamaliwa.
Majid alisema shitaka la kwanza linalowakabili washitakiwa hao ni kwamba Mei 12/2022 majira ya saa 8 Mchana katika Kijiji cha Isakamaliwa na kata ya Isakamaliwa wakiwa na nia ovu walimuuwa Darushi Bukwere (26) mkazi wa kata ya Isakamaliwa.
Shitaka la pili kwa washitakiwa hao ni kwamba katika Tarehe hiyo na muda huo katika kata hiyo ya Isakamaliwa wakiwa na nia ovu walimuua Gwisu-Manyenye (30) mkazi wa Kijiji cha Isakamaliwa.
Majid aliiambia mahakama kuwa shitaka la tatu linalowakabili washitakiwa ni kwamba katika Tarehe hiyo na muda huo washitakiwa wote kwa Pamoja walimuuwa Jacob Tungu (32) Mkazi wa kata ya Isakamaliwa.
Majid aliiambia mahakama kuwa washitakiwa wote walitenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 196 kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.
Hata hivyo Baada ya kusomewa mashitaka hayo matatu washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo ambapo kesi hiyo imeahilishwa hadi hadi machi 30/2023 itakapotajwa tena na washitakiwa wote wamepelekwa mahabusu.