Ndugu Wanahabari,

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linapenda kutoa taarifa kuhusiana na  kupatikana kwa mtoto aliyeibwa na tukio la watu wawili kuliwa na mnyama  Mamba wilayani Sengerema.

Tarehe 26.03.2023 muda wa saa 08:00 asubuhi, huko mtaa wa Migombani, Kata  ya Nyampulukano,Tarafa ya Sengerema, kuliripotiwa taarifa ya wizi wa mtoto  aitwaye Anitha Richard mwenye umri wa miezi 6 na mtu ambaye hakujulikana. 

Ni kwamba, Mama wa mtoto huyo aitwaye Agnes Robert, Miaka 26, Mkulima, na Mkazi wa Migombani alimuacha mtoto huyo kwa binti yake mdogo aitwaye  Martha Richard, Miaka 9 akiwa amembeba mgongoni kisha yeye kuingia bafuni  kwa ajili ya kuoga. 

Baada ya muda Martha, akiwa amembeba mdogo wake mgongoni aliitwa na jirani  yao aitwaye Costancia Deonatus na kumuagiza akiwa na watoto wenzake kufuata  ndoo yake kwa mtu aliyekuwa amenunua mkaa kwake ambaye jina lake  halikufahamika. 

Agnes Robert ambaye ni mama wa mtoto alipomaliza kuoga alitoka na kuanza  kuwatafuta watoto wake na ilipofika majira ya saa 13:00 mchana, watoto 02 walirejea nyumbani bila ya yule mwenzao wa miezi 06 aliyekuwa amebebwa mgongoni na dada yake, ndipo wazazi waliweza kugundua kuibiwa kwa mtoto  wao na kutoa taarifa kituo cha Polisi.

Baada ya tukio hilo kuripotiwa Askari Polisi walifanya msako mkali na kufika  katika kijiji cha Nyamaduke na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Happyness  William, miaka 18, mkulima na mkazi wa Nyehunge akiwa na mtoto huyo  aliyetambuliwa na wazazi wake kuwa ndiye aliyeibiwa katika kijiji hicho na baada  ya mahojiano ya kina mtuhumiwa amekiri kuhusika na tukio la wizi wa mtoto  huyo ambapo alidai kuwa alienda kumuonesha mumewe kuwa amejifungua. 

Upelelezi wa kesi hii unakamilishwa mara moja na mtuhumiwa atafikishwa  mahakamani haraka iwezekanavyo kukabiliana na mkono wa sheria. 

Tarehe 24.03.2023 muda wa saa 19:00 jioni huko mwalo wa Kazunzu, kijiji na  Kata ya Kazunzu, katika fukwe za ziwa Victoria kuliripotiwa taarifa ya mtu kuliwa  na mnyama Mamba. Askari Polisi kwa kushirikiana na wananchi walifika eneo  hilo ambapo ndugu waliweza kuutambua mwili wa mtu aliyekamatwa na kuliwa na  mnyama Mamba kuwa ni Salome Dotto miaka 30, mkulima na mkazi wa  Kazunzu.  

Mwili huo umefanyiwa uchunguzi na Daktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu  kwa taratibu za mazishi. 

Tarehe 09.03.2023 Muda wa saa 13:00 huko kijiji cha Izindabo, kata na tarafa ya  Buchosa wilaya ya sengerema, kuliripotiwa taarifa ya mtu mmoja aliyejulikana  kwa jina la Primitiva Evarist Miaka 56, Mkulima mkazi wa Izindabo,  aliyefariki baada ya kukamatwa na kuliwa na mnyama mamba wakati akinawa  miguu katika fukwe za ziwa victoria. 

Mwili wa Primitiva Evarist ulitambuliwa na ndugu na kufanyiwa uchunguzi  kisha kukabidhiwa kwa taratibu za mazishi. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kutoa rai kwa wazazi na walezi  kuendelea kuchukua tahadhari na kutimiza jukumu lao la msingi la uangalizi wa  watoto na sio kuwaacha peke yao bila uangalizi wa mtu mzima. Aidha, linawaasa  wananchi hususani wanaofanya shughuli zao katika fukwe za ziwa Victoria  kuchukua tahadhari ya usalama wao wenyewe ili kujiepusha na madhara  yanayoweza kujitokeza. Pia, linaomba kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili  ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka. 

Asanteni kwa kunisikiliza. 

Imetolewa na;-  

Wilbrod W. Mutafungwa- SACP  

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza