**************************************
MWENGE wa Uhuru uliokuwa unakimbizwa wilayani Ruangwa, mkoani Lindi umemaliza mbio zake na kukabidhiwa wilayani Nachingwea.
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Bw. Mzee Ali Mkongea amesema miradi mitatu ya maendeleo iliyopangwa kuzinduliwa wilayani humo, imeridhiwa na wataalamu wake.
Miradi hiyo ni mabweni mawili kwenye shule ye sekondari ya wasishana ya Hawa Mchopa, mradi wa maji wa Kitandi katika kata ya Likunja na mradi wa barabara ya lami kwenye kata ya Nachingwea, iliyoko Ruangwa mjini.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kupokea mwenge huo leo asubuhi (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) kwenye viwanja vya shule ya msingi Chiola, wilayani Nachingwea, Bw. Mkongea amewataka wananchi wa wilaya hiyo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na pia wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi huo, Novemba 24, mwaka huu.
Mapema, akizungumza na wakazi waliojitokeza kuupokea mwenge huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mwenge wa uhuru unakimbizwa maeneo mbalimbali nchini ili kuwahamasisha wananchi washiriki kwenye shughuli za maendeleo.
“Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kwenye maeneo yetu mbalimbali ili kuwahamasisha wananchi wajitokeze kushiriki kwenye miradi ya kujiletea maendeleo. Pia unaendana na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hivyo, tunakumbushwa kuyaenzi mawazo yake,” alisema.
Mbali ya kuwahimiza washiriki kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu alisema kuna makundi manne ambayo yanapaswa kushiriki uboreshaji wa taarifa zao kwenye Daftari la Mpiga Kura pindi zoezi hilo likianza.
“Wanaotakiwa kushiriki zoezi hili, ni wale waliopoteza vitambulisho vyao au wanavyo lakini vimefutika; waliohama maeneo yao na wako kwenye maeneo mapya ambako watapigia kura mwakani; waliokuwa na umri chini ya miaka 18 mwaka 2015 na sasa wamezidi umri huo; na wale ambao mwakani wanatarajia kufikisha umri wa miaka 18,” alisema.
Mapema, akizungumza baada ya kupokea mwenge huo saa 2:45 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Bi. Rukia Muwango alisema leo utakimbizwa kwenye wilaya hiyo ambapo miradi yenye thamani ya sh. milioni 781.5 itazinduliwa.
Kesho (Ijumaa, Oktoba 11) mwenge huo utaenda Liwale, Jumamosi (Oktoba 12) utaenda Kilwa na Jumapili (Oktoba 13) utakuwa Manispaa ya Lindi ambako utahitimisha mbio hizo na kuzimwa Oktoba 14, mwaka huu.