Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete akipokea toka kwa Rais wa Botswana Mhe. Mokgweetsi Masisi Tuzo ya Rais (Presidential Award) ya Mwaka 2023 inayotolewa na Taasisi ya Global Water Changemakers jijini New York, Marekani, leo.
****************************
Na Mwandishi Maalum, New York
Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ni miongoni mwa Viongozi Sita waliokabidhiwa Tuzo ya Rais (Presidential Award) ya Mwaka 2023 inayotolewa na Taasisi ya Global Water Changemakers.
Tuzo hiyo imetolewa kwa mara ya kwanza mwaka huu kwa Wakuu wa Nchi na Serikali 6 waliopo madarakani na waliostaafu kwa kutambua mchango wao katika kuonesha dhamira ya kweli ya kusimamia na kuleta mabadiliko chanya katika kuendeleza sekta ya maji katika nchi wanazotoka na barani Afrika.
Tuzo hizo zimekabidhiwa na Mhe. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Botswana katika Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Maji linaloendelea jijini New York, Marekani.
Viongozi waliopokea tuzo hizo ni Wenyeviti wenza wanne wa Jopo la Ngazi ya Juu la Kimataifa la Uwekezaji wa Maji kwa Afrika ambao ni Rais Macky Sall wa Senegal, Rais Hage Geingob wa Namibia, Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete wa Tanzania.
Aidha, tuzo hizo zimetolewa pia kwa Rais Hakainde Hichilema wa Zambia na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar kwa kutambua dhamira na uongozi wao kwenye kuendeleza sekta ya maji katika nchi zao. Zambia na Zanzibar ni nchi pekee zilizozindua Programu za Uwekezaji wa Maji barani Afrika.
Rais Mstaafu Kikwete amewawakilisha wenyeviti wenza hao watatu wa Jopo hilo katika Kongamano hilo. Pamoja na mambo mengine, Jopo lina wajibu wa kuratibu jitihada za kimataifa katika kukusanya fedha kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 30 ambazo ni pengo la ufadhili unaohitajika kutekeleza Mpango wa Uwekezaji wa Maji wa Bara la Afrika (AIP) utakaowezesha kutimiza lengo la Maendeleo Endelevu namba 6 la kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wote ifikapo mwaka 2023.
Takwimu zinaonyesha kuwa mmoja kati ya Waafrika watatu (takriban watu milioni 400) anakosa huduma ya maji safi ya kunywa huku watu wengine takriban milioni 700 wanaopata huduma hiyo hawana uhakika wa upatikanaji wake.