Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Mizengo Pinda akilakiwa na Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya baada ya kuwasili leo hii Kambarage House Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Geofrey Mizengo Pinda amefanya ziara Shirika la Nyumba la Taifa na kulakiwa na Menejimenti na Wafanyakazi wa Shirika.
Mheshimiwa Pinda amefanya ziara hiyo kufahamu kazi zinazofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuzungumza na Wafanyakazi wa Makao Makuu kwa niaba ya Wafanyakazi wote wa Shirika.
Akiwa NHC amelakiwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah Hamad na Wakurugenzi wengine na kisha kupokea wasilisho la Taarifa ya Mwenendo wa NHC na baadaye kuzungumza na wafanyakazi wa Shirika.
Baada ya mapokezi hayo Mkurugenzi Mkuu alimpeleka kwenye sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere na kumpa historia fupi ya sanamu hiyo kuwa lengo ni kuenzi mchango wa Mwasisi huyo wa Taifa kwa kuthamini makazi bora kwa wananchi wa Tanzania.
Akizungumza kumkaribisha Mheshimiwa Naibu Waziri, Hamad amemhakikishia Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa Shirika lina afya njema kiuchumi na kwamba limejipanga kukamilisha na kuanzisha miradi mipya kama ilivyo katika mpango mkakati wa Shirika.
“Mheshimiwa Naibu Waziri NHC inalo jukumu kubwa la kuwafanya Watanzania waweze kutabasamu kwa kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba na kuimarisha mipango ya upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu,”amesema.
Aliishukuru Serikali kwa kuliunga mkono Shirika la Nyumba la Taifa na kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwamo kukamilisha kazi za kikandarasi na kujenga kujenga majengo sambamba na kutoa ushauri wa kitaalamu wa ujenzi.
Mheshimiwa Mizengo Pinda atazungumza na Wafanyakazi mchana huu na kutoa maelekezo ya Serikali kwa ajili ya Shirika kuyatekeleza.