Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama akizungumza na watendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 196 zilizojengwa na WHI katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kujiridhisha na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 iliyotengwa na Serikali kuwezesha ujenzi wa nyumba hizo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifananua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 196 zilizojengwa na WHI katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakielekea kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 196 zilizojengwa na WHI katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kujiridhisha na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 iliyotengwa na Serikali kuwezesha ujenzi wa nyumba hizo.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria, Mhe. Edward Olelekaita Kisau akichangia hoja kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 196 zilizojengwa na WHI katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kujiridhisha na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 iliyotengwa na Serikali kuwezesha ujenzi wa nyumba hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI) Dkt. Fred Msemwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 196 zilizojengwa na WHI katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Katiba na Sheria wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa mradi huo.
Mwonekano wa baadhi ya nyumba zilizojengwa na Watumishi Housing Investments eneo la Njedengwa jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati yake, viongozi na watendaji wa WHI mara baada ya kamati hiyo kuhitimisha ukaguzi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba 196 zilizojengwa na WHI katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma.
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema kamati yake imeridhishwa na viwango vya nyumba 196 zilizojengewa na Watumishi Housing Investments (WHI) kwa kuzingatia kipato cha watumishi wa umma ili wapate makazi bora yatakayowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Dkt. Mhagama amesema hayo, wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati yake ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba 196 zilizojengwa na Watumishi Housing Investments (WHI) eneo la Njedengwa jijini Dodoma, lengo likiwa ni kujiridhisha na utekelezaji wa bajeti iliyotegwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 kuiwezesha WHI kutekeleza mradi huo.
Mhe. Dkt. Mhagama amefafanua kuwa, lengo kubwa la utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa nyumba katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma ni kuwawezesha watumishi wa umma kupata nyumba za bei nafuu ili waweze kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi zaidi.
Mhe. Dkt. Mhagama amesema, kamati yake imeridhishwa na hatua ya kukamilika kwa nyumba 196 katika kipindi cha muda mfupi na imefurahishwa na mwitikio wa watumishi wa umma kuzichangamkia nyumba hizo ambapo asilimia 94 ya nyumba hizo zimeshapata wanunuzi.
“Kitendo cha asilimia 94 ya nyumba 196 zilizojengwa WHI kupata wanunuzi kinaonyesha kuwa ujenzi wa nyumba hizo umezingatia hali halisi ya kipato na mahitaji ya watumishi wa umma na kuongeza kuwa, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anastahili kupongezwa kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo,” Mhe. Dkt. Mhagama amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, amekuwa akiisisitiza WHI kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuwawezesha kupata makazi bora ya kuishi.
Mhe. Jenista Mhagama amesema, ataendelea kuisisitiza WHI kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya watumishi wa umma nchini kwani ujenzi wake unapaswa kuhakikisha bei ya nyumba hizo unazingatia kipato cha watumishi wa umma kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Bei ya nyumba zinazojengwa na WHI zina upungufu wa asilimia 10 mpaka 30 katika soko la nyumba kama hizi ambazo zinajengwa na taasisi nyingine nchini,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments (WHI) Dkt. Fred Msemwa amesema, nyumba 196 zilizojengwa na taasisi yake zimezingatia mahitaji halisi ya familia za kitanzania pamoja na kipato chao.
Dkt. Msemwa amesema kuwa, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeridhishwa na viwango na bei ya nyumba hizo 196 zilizojengwa WHI kwa ajili ya kuwawezesha watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kupata makazi ya kuishi, hivyo wataendelea kujenga nyumba zinazozingatia mahitaji na kipato halisi cha Mtanzania.
Watumishi Housing Investments (WHI) inatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 1000 katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma, ambapo mpaka hivi sasa imekamilisha ujenzi wa nyumba 196 ambazo zimekaguliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.