Na. Asila Twaha, DAR ES SALAAM
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeipongeza Manispaa ya Kigamboni iliopo Mkoani Dar es Salaam kwa kujenga Kituo cha Afya kwa mapato ya ndani.
Pongezi hizo zimetolewa Machi 18, 2023 wakati Kamati hiyo ikifanya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ukiwemo utekelezwaji wa miradi wa kituo cha Afya Kibada kilichopo Manispaa ya Kigamboni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Mhe. Halima Mdee(Mb) amesema, lengo la ziara hiyo ni kujiridhisha na kufanya ukaguzi wa yale Serikali wanayoyasema upalekwaji na utekelezaji wa miradi kwa wananchi.
Amefafanua kuwa Manispaa ya Kigamboni imeonyesha mfano kwa kutenga fedha za mapato ya ndani na kujenga kituo cha afya ili wananchi waweze kupata huduma ni jambo ambalo linawagusa wananchi.
Amewataka watendaji Manispaa ya Kigamboni kuendelea kutumia mapato ya ndani kwa kuangalia vipaombele vya utoaji huduma bora wananchi.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho Dkt. Lucas Ngamtwa amesema, majengo yaliyojengwa mpaka sasa ni jengo la wazazi, jengo la upasuaji, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la kufulia, vyoo vya nje, shimo la kutupia kondo la nyuma pia ameleeza kuwa kituo hicho kitakuwa na jengo la mionzi ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza.
“ujenzi wa majengo yote ukikamilika utagharimu kiasi cha sh. milioni 640 ambapo fedha hizi zinazotokana na Mapato ya Ndani ya Halmashauri” Ngamtwa
Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya na kueleza vipo baadhi ya vifaa wameshatoa oda MSD ili visaidie kituo hicho.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) inaendelea na ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na mikopo ya 10%.