Muuguzi katika Hospitali ya wilaya Nyasa Lucia Lagila,akimsaidia mama aliyejifungua namna ya kunyonyesha mtoto.
Jengo la dharura.
********************************
SERIKALI imetoa shilingi milioni 800 kujenga Hospitali ya wilaya Nyasa,ili kusogeza na kuboresha huduma za afya kwa wananchi ambao awali walilazimika kwenda nje ya wilaya hiyo kufuata matibabu.
Kaimu Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Nyasa Dkt Simon Yasin alisema,katika ujenzi huo baadhi ya majengo ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje(OPD),wodi ya mama na mtoto na maabara yamekamilika na yameanza kutoa huduma.
Dkt Yasin ametaja huduma zilizoanza kutolewa katika Hospitali hiyo ni za wagonjwa wa nje,huduma ya mama na mtoto,kulaza wagonjwa na upasuaji.
“kwa sasa tuko katika awamu ya tatu na ya mwisho kabisa ya utekelezaji wake,katika awamu hii tunajenga jengo la upasuaji kwa wanawake na wanaume,jengo la kuhifadhia maiti sambamba na jengo la dharura ambalo limegharimu shilingi milioni 300”alisema Dkt Yasin.
Kwa mujibu wa Dkt Yasin,majengo hayo yatakapokamilika yatasaidia wananchi wa wilaya hiyo kupata huduma bora za matibabu,kuokoa vifo vya akina wakati na baada ya kujifungua na kupunguza muda wa kwenda maeneo mengine kufuata huduma za afya.
Alisema,Hospitali hiyo ni kubwa na imejengwa eneo ambalo kila mmoja rahisi kufika na imesaidia sana wananchi wa Nyasa kupata huduma za afya karibu.
Dkt Yasini,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita, kwa kuridhia kutoa fedha zilizotumika katika utekelezaji wa mradi huo muhimu na mkubwa kwa ajili ya wananchi.
Aidha alisema kuwa,kujengwa kwa Hospitali hiyo na kuanza kutoa huduma za matibabu kumewapunguzia wananchi kero na usumbufu wa kutembea umbali mrefu hadi katika Hospitali nyingine kufuata matibabu.
Ametoa wito kwa wananchi,kutumia zahanati,vituo vya afya na Hospitali zinazojengwa na serikali kwenda kupata huduma za matibabu kwa sababu zimejengwa kwa ajili yao.
Dkt Yasin,amewashauri akina mama pindi wanapohisi dalili za ujauzito ni vyema wakawahi kliniki mapema ili kupata ushauri kwa ajili ya usalama wao na mtoto aliyeko tumboni na wakati na baada ya kujifungua.
Kwa upande wake muuguzi wa Hospitali Lucia Lagila ametaja faida mojawapo kwa akina mama kuwahi kliniki ni kupunguza vifo vya mama na mtoto,kupata ushauri wa kitaalam wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Mkazi wa kijiji cha Ng’ombo Blandina Chalima alisema,kujengwa kwa Hospitali hiyo ni ukombozi mkubwa kwao kwani kwa muda mrefu walitegemea kupata huduma za matibabu kwenye zahanati moja tu inayomilikiwa na Kanisa.
Chalima,ameiomba serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Nyasa kuhakikisha inapeleka vifaa tiba na dawa za kutosha katika Hospitali hiyo,badala ya kuendelea kufuata baadhi ya huduma katika vituo vingine vilivyopo mbali na makazi yao.
Philip Chambo mkazi wa kijiji cha Kihagala,ameishukuru serikali kuboresha na kumarisha sekta ya afya kwani imesaidia kupunguza vifo vingi kwa wananchi katika wilaya hiyo.