Wauguzi na Wakunga wakila kiapo wakati wa mahafali ya saba na utoaji wa vyeti vya usajili na leseni kwa wauguzi na wakunga zaidi ya 1,000 waliofanya vizuri kwenye mitihani iliyoandaliwa na Baraza la Uuguzi na Ukunga (TNMC) jana jijini Dodoma.
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini (TNMC) Agnes Mtawa mwenye suti nyeusi pamoja na Mwenyekiti wa baraza hilo Prof. Lilian Mselle, wakiwasha mshumaa jana jijini Dodoma wakati wa mahafali ya saba na utoaji wa vyeti vya usajili na leseni kwa wauuguzi na wakunga ikiwa ni tendo la kuashiria upendo kwa wagonjwa wanao wahudumia.
PICHA PAUL MABEJA
Na Paul Mabeja,DODOMA
MSAJILI wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) Agnes Mtawa, amesema vitendo vya uvunjifu wa maadili, pamoja na wauguzi na wakunga vishoka ambao wamekuwa wakijiingiza katika taaluma hiyo bado ni kikwazo katika sekta ya afya nchini.
Mtawa, alibainisha hayo jana jijini Dodoma, wakati wa mahafali ya saba na utoaji wa vyeti vya usajili na leseni kwa wauguzi na wakunga zaidi ya 1,000 waliofanya vizuri kwenye mitihani iliyoandaliwa na TNMC.
“Pamoja na mafaniko tuliyoyapa lakini bado zipo changamoto mbalimbali ikiwemi vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa wauguzi na wakunga, lakini pia lipo tatizo la watu ambao siyo wanataaluma kuingilia taaluma yetu”alisema
Aidha, alisema wauguzi na wakunga wanapaswa kuzingatia maadili ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza katika maeneo mbalimbali ili kuisaidia serikali kupunguza vifo vya mama na mtoto.
“Sisi tutaendelea kuchukua hatua kwa muuguzi au mkunga yeyote ambaye atabainika kuwa amekiuka maadili kwa kumfuta kwenye usajili wetu”alisema
Vile vile, alisema tangu mwaka 2016 wauguzi na wakunga 50 walibainika kuvunja maadili ya utumishi wa umma ambapo kati yao wanne walifutiwa usajili wao na kupokonywa leseni na wengine kupewa kalipio kali.
Pia, alisema pamoja na kero hiyo ya ukiukajai wa maadili ya kada hiyo lakini bado ipo kero ya wauuguzi na wakunga vishoka ambao siyo wanataaluma.
“Bado wapo wananchi ambao wanajifanya wanataaluma hii na kutoa huduma bila ya kuwa na vigezo hili ni kosa la jinai ambao tumekuwa tukiwabaini tumewachuklia hatua za kuwapeleka mahakamani na wengine tayari wameshafungwa vifungo mbalimbali”alisisitiza Mtawa
Kadhalika, alisema ili kukabilina na kero hiyo Baraza limeandaa mfumo ambao limewapatia waajiri ili waweze kuhakiki usajili ya wauguzi na wakunga.
“Mfumo huu unaouwezo wa kubaini muuguzi au mkunga aliyesajiliwa na asiye sajiliwa hivyo nitoe wito kwa waajiri kufanya uhakiki kupitia mfumo huu mara kwa mara ili kukabili changamoto ya watu wasio wanataaluma kujipenyeza”alisema
Alisema hadi sasa waunguzi na wakunga waliosajiliwa nchini ni 55,000 lakini wenye leseni zilizo hai ni 42,000 ambao wanatoa huduma katika vituo mbalimbali vya serikali na binafsi.
Muuguzi mkuu wa serikali, Ziada Sellah aliwataka wauuguzi na wakunga kuacha tabia ya kuchangia maeneo ya kwenda kufanya kazi.
Alisema wanapaswa kufahamu kuwa watu wenye mahitaji wapo nchi nzima hivyo hawanabudi kuchagua maeneo ya mijini kwenda kufanya kazi.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Lilian Mselle alisema wataendelea kuchukua hatu kwa mtumishi yeyote ambaye ataoneka kuitia doa taaluma hiyo kwa kufanya vitendo vya uvunjifu wa maadili.