Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin J. Rwezimula ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali ya Uholanzi na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza sekta ya elimu na kukuza ujuzi kwa vijana ili kuweza kuwapitia elimu itakayowawezesha kujiari.
Amesema hayo katika hafla ya kukamilika kwa mradi wa Orange Knowledge Programme (OKP) iliyofanyika katika ukumbi wa HORTI -Tengeru jijini Arusha Tarehe 17, Machi, 2023.
Dkt. Franklin amesema kupitia mradi huu vijana wamenufaika kwa kupata mafunzo na ujuzi katika kilimo cha matunda na mboga mboga (Horticulture), ujenzi wa miundombinu, na vifaa mbalimbali vitakavyowasaidia kujikwamua na changamoto ya ajira.
Hivyo Wizara itahakikisha mafunzo na ujuzi uliopatikana unakuwa endelevu na kuhakikisha vyuo vyote vya Ufundi vinatoa elimu yenye ubora ili kusaidia vijana na taifa kwa kupata nguvu kazi yenye maujuzi unaohitajika ka soko la ajira.
Kwa upande wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Kaimu Katibu Mtendaji Dkt. Amani Makota amesema kuwa pamoja na manufaa mbalimbali ya mradi huo, walimu pia wameweza kupata mafunzo ambayo yamesaidia kuwajengea uwezo na ufanisi katika ufundishaji pamoja na uboreshwaji wa mitaala.
Mradi huo uliofadhiliwa na serikali ya Uholanzi na kusimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mfunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Maastricht Uholanzi ulikua na lengo la kusaidia kuboresha kilimo cha matunda na mboga mboga nchini.
Vyuo vilivyonufaika na mradi huo ni pamoja na MATI Uyole – MBEYA, HORTI – Tengeru na Mahinya Institute of Sustainable Agriculture- Songea