Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amezitaka kampuni za madini nchini kuendelea kutoa elimu na kuwajengea uwezo watanzania na wamiliki wa kampuni za kitanzania ili waweze kushiriki katika mnyororo wa shughuli za madini hasa kwenye utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.
Profesa Kikula ametoa rai hiyo leo Machi 17, 2023 jijini Arusha alipokuwa akifunga Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini lililofanyika kwa siku tatu na kukutanisha kampuni za uchimbaji wa madini, watoa huduma kwenye migodi ya madini na Taasisi za Kifedha.
Amesema kuwa ili kuhakikisha wananchi wanatumia fursa za utoaji wa huduma zilizopo kwenye migodi ya madini kama vile usambazaji wa vyakula, ajira, ulinzi, ni vyema kampuni za utafiti na uchimbaji wa madini zikaendelea kutoa elimu kwa jamii inayozunguka ikiwa ni pamoja na fursa, viwango vya huduma vinavyotarajiwa ili wananchi waweze kushiriki na kujipatia kipato huku Serikali ikipata mapato yake.
Profesa Kikula amezitaka kampuni za madini, watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa kuzingatia viapo vya uadilifu wanavyowasilisha Tume ya Madini kwa kuendesha shughuli zao.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amezitaka kampuni za kitanzania zinazofanya kazi katika migodi mbalimbali kuwa waaminifu na hivyo kutengeneza fursa zaidi kwa watanzania wengine.
“Ni vyema kampuni za kitanzania zinazopewa kazi kwenye migodi ya madini kwa kuaminiwa zikahakikisha zinatoa huduma kulingana na viwango vinavyotarajiwa na kampuni za madini na kwa uaminifu wa hali ya juu ili kufungua fursa kwa kampuni nyingine za kitanzania kwa kuendelea kuaminiwa,” amesema Profesa Kikula.
Ameendelea kusema kuwa kama mkakati wa kutatua changamoto za watoa huduma kwenye migodi ya madini, Serikali kupitia Tume ya Madini itaendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini ikiwa ni pamoja na majukwaa mbalimbali yenye lengo la kubadilishana uzoefu, kujadiliana changamoto mbalimbali pamoja na kuzitatua.
Wakati huohuo, Profesa Kikula amepongeza wadhamini wa jukwaa hilo kwa kufanikisha kwa kiasi kikubwa maandalizi yake pamoja na kuwakabidhi tuzo mbalimbali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau wa madini kwenye ufungaji wa jukwaa hilo wameipongeza Tume ya Madini kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini hasa kwenye uhamasishaji wa wachimbaji kutokutumia zebaki kwenye uchenjuaji wa madini na ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.