Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akieleza utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya kisangara mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii, ilipofanya ziara kwenye Kampasi hiyo iliyopo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Dkt Gwajima akijadiliana jambo na Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi Kisangara, Mkoani Kilimanjaro
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii Bi Fatma Tawfiq akizungumza wakati ziara ya kamati hiyo katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Kampasi ya Kisangara, mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kukagua miradi ya Maendeleo
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt John Jingu akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii ya kukagua Miradi ya Maendeleo katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangar, Mkoani Kilimanjaro
Viongozi na wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakiwasili katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, kampasi ya kisangara, Machi 16, 2023 Mkoani Kilimanjaro.
Na Abdu Madenge-MJJWM, KILIMANJARO
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya jamii imefurahishwa na ukuaji wa kasi wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Kampasi ya Kisangara, wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.
Hali hiyo imebainika kufuatia Ziara ya Kamati hiyo yenye lengo la kujionea utekelezaji wa Majukumu na Miradi ya Maendeleo katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara, Machi 16, 2023.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Fatma Tawfiq pamoja na mambo mengine amesema Kamati itaendelea kuishawishi Serikali kutenga fedha kwa ajili ya Taasisi hiyo ili kuchochea Morali na kasi ya ukuaji wake ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa udahili kwa asilimia 300.
“Nikipongeze sana chuo hiki kwa jitihada nzuri na kubwa mnazofanya, hasa suala la kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 56 mwaka 2016/17 hadi wanafunzi 245 mwaka 2022/23,” amesema Mhe. Fatma Towfiq.
Mwenyekiti Tawfiq ametumia fursa hiyo kuushauri uongozi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii kuhakikisha wanapata Hati ya umiliki wa eneo la Kampasi hiyo kwa kushirikiana na Uongozi wa eneo husika ili kuepuka uvamizi.
Aidha Mhe. Tawfiq ameitaka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kampasi ya Kisangara kuweka Mkakati wa kutumia Mapato ya ndani kwa kujenga nyumba za wahadhiri na watumishi wa Taasisi hiyo.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Taasisi hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt.Dorothy Gwajima amesema lengo la Taasisi ni kuhakikisha inaboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ili kuongeza uwezo wa kudahili hata kufikia wanafunzi 800.
Dkt . Gwajima ametumia fursa hiyo kubainisha mpango wa Taasisi wa kuandaa mtaala wa Elimu ya Malezi na makuzi ya mtoto katika ngazi ya cheti hadi ngazi ya stashahada na suala na kuongeza idadi ya wahadhiri.
“Chuo kimepata kibali cha kuajiri waadhiri wengine 8 ambapo mchakato wa ajira bado unaendelea na utazingatia usawa wa kijinsia, mahitaji Maalum na pia uwezo wa kitaaluma katika kufundisha ” amesema Dkt. Gwajima
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ameahidi kufanyiwa kazi maelekezo yaliyotolewa na Kamati ikiwemo suala la upungufu wa watumishi.
Naye Diwani wa kata ya Lembeni Mhe. Alex Mwipopo amesema mwanzo chuo hicho kilikua ni kama kimeshaulika lakini ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita chuo hiko kimeongeza fursa kubwa kwa wananchi wa kata hiyo kiuchumi na kimiundombinu huku kila mtu akiona shauku ya kuhamia kwenye eneo hilo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na fursa zinazopatikana.