Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutoa elimu nchini.
Waziri Mkenda ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa huduma ya mkopo wa Elimu inayotolewa na Benki ya NMB.
Amesema kinachofanyika na Benki ya NMB ni kuonyesha njia kwa kuwa pamoja na kuanzisha mkopo wa elimu wamekuwa wakitoa ufadhili wa masomo ambapo kwa mwaka huu wamenufaisha wanafunzi 100.
“Mwaka jana Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB alikuja ofisini kwangu akasema tunataka kuunga mkono juhudi za Serikali na tunachagua eneo ambalo Mhe Rais ameelekeza nguvu kubwa kwa kutenga Sh bilioni 200 na kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 100 na leo ni siku ya furaha kufanya uzinduzi huu kuongeza fursa ya watu kupata mikopo kwa ajili ya elimu” amesema Prof. Mkenda
Mkenda amewataka NMB kuhakikisha wanatangaza fursa hii kote nchini ili iwanufaishe watanzania wengi na kusisitiza kuwa mikopo ya NMB itolewe si kwa ajili ya Elimu juu pekee bali hata kwa wanaosoma vyuo vya kati.
Aidha ametoa wito kwa wahitimu wa shule mbalimbali kushiriki kuchangia maendeleo ya elimu hususan katika kuchangia maendeleo ya shule walizosoma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema uzinduzi wa mkopo wa elimu ambao umefanyika leo na NMB kwa kushirikiana na wizara ni jambo jema kwa kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu haijawahi kutosha kwa kuwa mtoaji amekuwa ni Serikali kuu pekee.
Ametoa wito kwa Taasisi nyingine za kifedha kuiga jambo hilo zuri kwa kuwa ndivyo inavyofanyika duniani kote kuwa anaetoa mkopo si Serikali peke yake.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ameishukuru Menejimenti ya Benki ya NMB kwa kubaini hitaji kubwa la gharama za elimu kwa wazazi, walezi na vijana nchini na kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kuongeza fursa ya upatikanaji wa fedha kupitia mkopo wenye riba nafuu.
“Kwetu sisi Benki ya NMB ni zaidi ya mdau wa elimu kwa sababu ya ushiriki wake wa mara kwa mara katika kuleta afua za kifedha kwenye Sekta ya elimu,”amesema Prof. Carolyne Nombo
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Ruth Zaipuna amesema benki hiyo imetenga Sh Bilioni 200 kwa ajili ya kugharamia elimu ikiwa ni kuendeleza juhudi za Serikali katika kukuza Sekta ya Elimu hapa nchini.
Zaipuna ameongeza kuwa mkopo huo wa elimu utakuwa wa riba nafuu asilimia 9, utatolewa kwa watumishi na wafanyakazi ambao mishahara yao inapita NMB na kuongeza kuwa mteja anaruhusiwa kukopa kuanzia laki mbili hadi milioni 10 na kwamba utatolewa kwenye matawi yote ya NMB.
“Kuanzia leo, tumeanza rasmi kupokea maombi ya mikopo kwa watumishi ambao mishahara yao inapita Benki ya NMB, na inaweza kuchukuliwa kwa ajili ya mhusika mwenyewe kujiendeleza kielimu ama kwaajili ya vijana, ama Watoto wao hata wenza wao”,amesema Zaipuna