***********************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer amekabidhi mifuko 100 ya saruji kati ya mifuko ya 200 aliyoahidi kwa ajili ya kujengea bweni la shule ya msingi Saniniu Laizer.
Kiria amekabidhi mifuko hiyo ya saruji kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Swedefrida Msoma, iliopo kitongoji cha Namelock kijiji cha Naepo kata ya Naisinyai.
Akizungumza baada ya kukabidhi mifuko hiyo 100 ya saruji, Kiria amesema itasaidia kuanza ujenzi wa bweni la shule hiyo kwa ajili ya kulala wanafunzi wanaotoka mbali ili kufika shuleni.
“Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro iliahidi kujenga bweni hivyo nikajitolea mifuko 200 kwa ajili ya kusaidi aujenzi huo wa bweni hivyo tumetanguliza 100 kisha tutamalizia 100 iliyobaki,” amesema Kiria.
Mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi Saniniu Laizer, Swedefrida Msoma, amemshukuru Kiria kwa kujitolea matofali hayo 100 kati ya 200 alioahidi kutoa kwao.
“Tunamshukuru na kumpongeza Kiria kwa kujitolea mifuko hiyo ya saruji 100 itakuwa mwanzo mzuri wa kujenga bweni la wanafunzi wa shule hii, wakati tunasubiri mifugo mingine 100,” amesema Msoma.
Shule ya awali na msingi Saniniu Laizer ya mchepuko wa kiingereza ipo kitongoji cha Namelock kijiji cha Naepo kata ya Naisinyai, imejengwa na bilionea Laizer kwa gharama ya sh466.8 milioni na kuikabidhi Serikali Januari 2021.