Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Costantine Kanyasu (katikati) akikagua maeneo ya kituo cha pembe nne za utamaduni (4CCP) Haydom.
Msanii Paschal Daniel wa Pamoja Central Group wa Mwanza akizungumza kwenye tamasha la nane la utamaduni Haydom.
**************************
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu amehitimisha tamasha la nane la utamaduni Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, lililokutanisha makundi makuu manne ya lugha za Afrika, kwa kuitaka jamii ithamini utamaduni kwani una uwezo mkubwa wa kukuza utalii.
Kanyasu aliyasema hayo kwenye tamasha la nane la pembe nne za utamaduni Haydom (4CCP) lililojumuisha vikundi vya sanaa vya mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alisema utamaduni una nguvu kubwa ya kuongeza watalii wengi hapa nchini kwani ni kivutio ambacho hakichoshi kuangalia kila wakati hivyo fursa hiyo ichangamkiwe.
“Kuna nchi hazina mbuga, hifadhi, wala wanyamapori lakini wanapata watalii wengi kutokana na utamaduni walionao kwani unaweza kumuona tembo na kisha usirudi tena mwakani lakini utamaduni utarudi kila mwaka,” alisema.
Mratibu wa 4CCP Eluminatha Awet alisema Haydom ni kitovu cha Afrika kwani ni sehemu pekee inayokutanisha tamaduni nne tofauti na kuziweka mahali pamoja.
Awet alisema jamii nne Afrika za wanailotiki (datoga), wakushiti (iraqw), wakhoisans (wahadzabe) na wabantu wamekutana kwenye tamasha hilo.
“Makundi makuu ya lugha za Afrika yamekutana mahali hapa licha ya tofauti zao za lugha, mfumo wa maisha, tamaduni na hata shughuli za kiuchumi,” alisema.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga alisema kituo hicho cha utamaduni kimeasisiwa na raia wa Norway marehemu Dk Halgrim Olsen.
Mofuga alisema marehemu Dk Olsen alifanya maendeleo mengi enzi ya uhai wake ikiwemo ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Haydom na kituo cha polisi Haydom.
Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Massay alisema naye ni miongoni mwa waanzilishi wa tamasha hilo akiwa msanii wa Tumaini sanaa group.
Massay aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwapatia mizinga ya nyuki 100 ambayo waliikabidhi jamii ya wahadzabe wa bonde la Yaeda Chini.
Mkazi wa Haydom Elias Bura amepongeza hatua ya 4CCP kuandaa jambo hilo la kihistoria ambalo huu ni mwaka wa nane tangu waanzishe.
“Tumeona ngoma, kurusha mishale, mikuki, kuchapana, nyumba zao, mavazi na vyakula vya utamaduni tofauti ya jamii kubwa nne za Afrika hapa Haydom,” alisema.
Tamasha hilo limefanyika kwa siku nne na kuhusisha vikundi 15 vya sanaa za ngoma kutoka mikoa ya Manyara, Arusha, Singida na Mwanza.