NA FARIDA MANGUBE KILOSA MOROGORO.
Wakazi wa kijiji cha Masungo Kata ya Mtumbatu wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, wanakabiliwa na changamoto ya kituo cha Afya hali inayosababisha akina mama wajawazito na watoto kupoteza maisha kwa kushindwa kupata huduma kwa haraka wakilazimika kufuata huduma za afya kijiji jirani .
Wakizungumza wakati wakuchimba msingi wa jengo la Zahanati ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani wananchi wa kijiji hicho akiwemo Bi. Lozza Senyagwa alisema wameamua kusherekea siku ya wanawake kwa kuchimba msingi wa zahanati ili kunusuru vifo vya wajawazito wanapoteza maisha kwa kufuata huduma ya afya zaidi Kilometa tano.
“tumeona ni vyema tukaitumia siku ya wananwake Duniani kuchimba msingi wa Zahaati kama sehemu ya kuadhimisha siku hii muhimu kwetu.” Alisema bi. Lozza.
Nae Ally Segua mkazi wa Kijiji cha Masongo alisema kilio kikubwa kwenye eneo hilo ni Zahanati hivyo kuanza kuchibwa kwa msingi kunaonyesha njia ya matumaini ya kuondokana na changamoto ya kukosa huduma bora za afya.
Aidha ameiomba Serikali ya Rais Samia kupitia watendaji wa Serikali na viongozi wa chama cha Mapinduzi kuwekeza nguvu ya kutosha katika kujenzi wa Zahanati na wananchi wapate huduma ya afya karibu na maeneo hayo.
Kwa upade wake Diwani wa kata ya Mtumbatu Bwana.Amani Sewando alisema katika kuunga mkono juhudi za wananchi wa kijiji hicho ametoa mifuko 50 ya saruji pamoja na kushiriki zoezi la uchimbaji wa msinga kama sehemu ya mchango wake.
Alisema ujenzi wa Zahanati hiyo unakwenda kuokoa maisha ya wanawake wajawazito na watoto wachanga kwani toka kuanzishwa kwa kijiji hicho miaka 17 iliyopita hakukuwa na huduma bora za afya.
Aidha ameomba serikali kuu kuunga mkono juhudi zilizofanywa na wananchi wa kjiji hicho kuanzisha ujenzi wa Zahanati na kwamba ujenzi huo utakapo kamilika wananchi hao wapelekewe vifaa tiba pamoja na wauguzi.